Na Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Timu ya mpira wa
miguu wanaume ya Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga (Mahakama FC) imejipima ubavu
na timu ya mpira wa miguu wanaume ya Halmashauri ya Ushetu (Watumishi FC)
kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa mwishoni mwa juma.
Katika mchezo huo
uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kom iliyopo katika Manispaa
ya Shinyanga, Watumishi FC kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Ushetu iliibuka
washindi baada ya kuwabamiza Mahakama FC bao 1-0.
Bao hilo
lilipachikwa kimyani katika dakika ya 28
ya kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao, Mwl. Rashid Kilingamoyo.
Katika kipindi cha
kwanza, timu ya watumishi FC ilionekana kuchungulia mara kwa mara lango la
Mahakama FC. Hata hivyo, golikipa wa Mahakama FC, John Japhet aliokoa mikwaju
kadhaa iliyokuwa ikielekezwa langoni kwake.
Mashambulizi zaidi
yalielekezwa kwenye lango la Mahakama FC ambapo katika dakika ya 43 ya mchezo,
mchezaji wa Watumishi FC, Bazil Bazil aliachia shuti kali lililogongwa mwamba
na kutoka nje ya uwanja. Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Watumishi FC
walikuwa wanaongoza kwa bao moja kwa nunge.
Kipindi cha pili
kilianza kwa kasi ambapo Mahakama FC ilionekana kujipanga vyema baada ya
kufanya mabadiliko katika safi ya ushambiliaji ambapo Hamza Mrutu alichukua
nafasi ya Gustafu na kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Watumishi FC.
Timu zote
zilionekana kushambuliana kwa zamu kwani kila mmoja tayari alikuwa amewasoma wapinzani
wake na mashambulizi yalielekezwa katika pande zote. Hadi dakika tisini za
mchezo zinakamilika, Watumishi FC waliibuka washindi baada ya kuwafunga kwa
mbinde Mahakama FC kwa bao 1 – 0.
Akiongea baada ya
mchezo huo wa kirafiki kukamilika, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Lunguya
Kahama, ambaye pia ni mchezaji wa Mahakama FC, aliipongeza timu ya Watumishi FC
kwa kukubali kusafiri hadi mjini Shinyanga kushiriki katika mechi hiyo ya
kirafiki.
Alisema mchezo huo
ni hatua mojawapo waliyoichukua kuandaa timu ya Mahakama FC ambayo itashiriki Bonanza kubwa la Michezo
mwezi Novemba, 2023 linalotarajiwa kufanyika mjini Bukoba.
“Kupitia mechi
hii, tayari sisi Mahakama FC tumejipima na tumeona ni wapi ambapo tunahitaji
jitihada zaidi ili tuendelee kuimarika, niwapongeze sana Watumishi FC kwa
ushindi wa bao 1 – 0 dhidi ya Mahakama FC, nasi tunaendelea kujipanga, tutawafuata
Ushetu,’’ alisema.
Naye Katibu wa
Watumishi FC, Mwl. Hamad Sule aliushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Shinyanga kwa kukubali timu hizo kushiriki mechi hiyo ya kirafiki ambayo kwa
namna nyingine imezidi kuimarisha mahusiano baina ya Watumishi wa Mahakama na
Watumishi wa Halmashauri.
“Niwapongeze sana,
timu iko vizuri sana, katika historia ya timu yetu hatujawahi kumfunga mtu bao
chini ya tatu, hivyo nyinyi mko vizuri, niwapongeze sana. Michezo ni afya, michezo
ni furaha, michezo inaimarisha mahusiano baina miongoni mwa watumishi wa umma,’’
alisema.
Mahakama FC inaendelea na mazoezi yake kuelekea Bonanza la michezo litakalofanyika Bukoba, litakalojumuisha Kanda tano za Mahakama Kuu ambazo ni Bukoba (Mwenyeji), Mwanza, Shinyanga, Musoma na Tabora.
Kikosi cha timu ya
mpira wa miguu (Mahakama FC) cha Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga katika picha
ya pamoja.
Kikosi cha timu ya
mpira wa miguu (Watumishi FC) cha Halmashauri ya Ushetu, Kahama katika picha ya
pamoja.
Timu za Mahakama
FC ya Shinyanga na Watumishi FC ya Ushetu katika picha ya pamoja.
Mshambuliaji wa
Mahakama FC Hamza Mrutu akiwa katika jukumu la kuhakikisha mashambulizi dhidi
ya watumishi FC ni ya moto.
Kocha wa Mahakama FC, Bw. Abdulmuuminu Mbaraka akiongea na wachezaji wa Mahakama FC (hawapo katika picha) wakati wa mapumziko.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni