Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza
Mahakama
ya Tanzania katika ukanda wa Ziwa Victoria imeandaa Bonanza la michezo litakaloshirikisha
Kanda tano za Mahakama Kuu Bukoba, Mwanza, Shinyanga, Musoma na Tabora ambalo
litafanyika mwezi Novemba, 2023 mjini Bukoba.
Kufuatia
hatua hiyo, timu ya Mahakama Mkoa wa Mwanza imeendelea na mazoezi yake katika
viwanja vya Shule ya Sekondari Bidii kwa ajili ya kujiweka sawa tayari kwa
ajili ya Bonanza hilo.
Akiongea
na Mwakilishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Msemaji wa timu za Mahakama katika Mkoa
huo, Edward Ntambi alisema kuwa maandalizi yanaendelea vema ili kupata namba ya
kuridhisha ya washiriki katika michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu na
mpira wa pete.
“Pamoja
na kuwa tunategemea wachezaji wengine waliopo katika Wilaya nyingine za Mkoa wa
Mwanza, watumishi waliopo Ilemela na Nyamagana wameendelea kujitokeza na
kushiriki mazoezi haya,” alisema.
Alisema
wachezaji wameendelea kujifua katika michezo ya mpira wa miguu, riadha, mpira
wa wavu, mpira wa pete na ‘draft’ huku ikitegemewa idadi ya michezo itaongezeka
kadri washiriki watakavyokuwa wakiongezeka. Hatua hiyo itatoa fursa kwa
watumishi wengi kushiriki angalau mchezo mmoja kwa ajili ya kuweka mwili na
akili sawa.
“Kuna
wachezaji mahiri na hatari ambao wakiungana na hawa wanaoendelea na mazoezi
sasa. Ninaamini timu za Mahakama Mkoa wa Mwanza zitabeba vikombe vyote. Waandaji
waandae medali za kutosha maana hatutachaa kitu huko Bukoba katika Bonanza hilo.
Hiki kinachoendelea ni rasharasha, mvua kamili itashuka kuanzia mwezi ujao,”
alijitapa msemaji huyo.
Bonanza hilo kwa Mahakama za ukanda wa Ziwa Victoria, kwa mara ya kwanza lilifanyika mkoani Mwanza mwaka jana ambapo timu kutoka Mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga zilishiriki. Kwa mwaka huu itakuwa ni mara ya pili ambapo idadi ya Mikoa itakayoshiriki inategemewa kuongezeka zaidi, hivyo kuvutia watumishi wengi kushiriki Bonanza hilo kwa ajili ya kuweka miili yao sawa.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mwanza Mjini, John Mngonya akimiliki mpira tayari kwa kufunga goli wakati wa mazoezi hayo.
Wachezaji wa mpira
pete wa timu ya Mahakama Mkoa wa Mwanza wakiendelea na mazoezi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni