Jumanne, 29 Agosti 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA MUSOMA WAFANYA UTALII WA NDANI

Na. Francisca Swai-Mahakama, Musoma

Watumishi pamoja na Viongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma hivi karibuni walitembelea na kufanya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Grumeti iliyoko wilayani Serengeti.

Hifadhi ya Grumeti inapatikana katika ukanda wa Magharibi wa mfumo wa ikolojia ya Serengeti na ilianzishwa mwaka 2002. Hifadhi hiyo ipo katika eneo linalotenganisha (buffer zone) Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo ya makazi ya wananchi.

Wakiwa katika ziara hiyo, watumishi hao walipata fursa ya kuonana na uongozi ambao walielezea uzuri wa hifadhi hiyo, ikiwemo uwezo wa kuwaona wanyama watano wakubwa duniani (the big five) ambao ni Tembo, Simba, Chui, Nyati na Faru pamoja na wanyama wengine wengi ndani ya muda mchache.

Viongozi hao, Meneja Mkuu Utafiti na Huduma za Jamii, Bw. Noel Mbise, Meneja wa Kitengo cha Mahusiano Grumeti, Bw. David Mwakipesile na Mtaalam wa GIS, Bw. Exavery Kigosi pia walieleza jinsi Hifadhi ya Grumeti ilivyo na uhifadhi bora wa wanyama katika eneo hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, TAWA, TANAPA pamoja na jamii inyozunguka.

Wataalamu hao walieleza kuwa, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa katika kulinda na kuhifadhi mazingira na wanyama kwa ujumla wake bado wanarudishwa nyuma kwa kiasi kikubwa na uwepo wa matukio ya ujangili kutokana na eneo hilo kuwa ‘buffer zone’ karibu na makazi ya wananchi.

Watumishi wa Mahakama ambao waliongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, waliweza kujionea na kuufurahia uzuri wa nchi ya Tanzania kwa kushuhudia namna wanyama wanavyoweza kuishi katika mazingira yao kwa uhuru, licha ya kuwa mazingira ya hifadhini yanaongozwa na mwenye nguvu (survival of the fittest).

Baada ya utalii huo ,watumishi hao walionekana kufurahi na kuahidi kuendelea kutembea maeneo mengine ya nchi kadri nafasi itakavyoruhusu ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada kubwa za Serikali katika kutangaza vivutio mbalimbali nchini.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma walioshiriki ziara ya utalii katika hifadhi ya Grumeti wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (mwenye koti la rangi ya bluu) wakifurahi kwa pamoja.

Meneja Mkuu Utafiti na Huduma za Jamii, Bw. Noel Mbise (aliyesimama) akitoa maelezo mbalimbali kuhusu Hifadhi ya Grumeti. Wengine katika picha ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya wa kwanza kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Marlin Komba (katikati).

Meneja wa Kitengo cha Mahusiano Grumeti, Bw. David Mwakipesile akielezea namna shughuli za uhifadhi zinavyofanyika na namna hifadhi inavyojitahidi kukabiliana na ujangili katika Hifadhi ya Grumeti.

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Hifadhi ya Grumeti kabla ya kuanza ziara ya utalii.

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma wakipata maelezo ya namna ambavyo wanatakiwa kuwa na utulivu na kuenenda wakati wote kabla ya kuanza utalii wenyewe.

Watumishi wakifurahia utalii katika hifadhi ya Grumeti.

Kundi la Tembo likipita mbele ya magari yaliyobeba watumishi wakati wa utalii.

Sehemu ya wanyama walioonekana katika hifadhi ya Grumeti.

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma wakisikiliza kwa makini maelezo ya Mtaalam wa GIS, Bw. Exavery Kigosi (aliyesimama) kuhusu shughuli za uhifadhi na huduma za kijamii zinazotolewa na Hifadhi ya Grumeti.

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma wakiwa katika picha ya pamoja kwa furaha na uongozi wa Grumeti baada ya kuhitimisha ziara ya utalii katika hifadhi ya Grumeti.

 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni