Jumatano, 30 Agosti 2023

UPUNGUFU WA WATUMISHI UTUMIKE KAMA FURSA YA KUJIFUNZA KAZI NYINGINE; JAJI DKT. MASABO

Na Eva J. Leshange, Mahakama-Singida

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amewaasa watumishi wa Mahakama wilayani Iramba kutumia fursa ya upungufu wa watumishi kwa kujifunza kazi nyingine na kuongeza maarifa zaidi na kwakuwa rasilimali watu haijawahi kutosha. 

 Mhe. Dkt. Masabo aliyasema hayo hivi karibuni akiwa katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi Wilayani Iramba.

 “Ndugu watumishi upungufu wa watumishi uwe ni fursa kwenu ya kuelewa majukumu mengine ili kujijengea uwezo, dunia inaenda kasi hivyo ni lazima kujifunza vitu vipya” alisema.

Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza watumishi hao kuzingatia uadilifu, weledi, uwajibikaji, kujiendeleza kielimu na  kutumia vizuri fursa inayotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuhudhuria mafunzo yanayofanyika kwa njia ya mtandao ili kukuza maarifa zaidi. 

Aliongeza kwa kushauri kuwa, kila Mkoa unaweza kuandaa mafunzo ya ndani hata ya ujasiriamali kwani kuna maisha mengine zaidi ya ajira tulizo nazo.

Aidha, aliwapongeza Mahakimu pamoja na watumishi kwa kazi nzuri wanayofanya hasa katika usikilizaji wa mashauri.

Akipokea taarifa iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama Wilaya Iramba, Mhe. Luzango Khamsini  kwenye kipengele cha mashauri ya mlundikano, Mhe. Dkt. Masabo alielezwa kwamba, Mahakama hiyo ina mashauri mawili (2) pekee ya mlundikano.

Hata hivyo, Jaji Mfawidhi amewasisitiza kuongeza kasi zaidi na kuhakikisha hakuna kabisa kesi za mlundikano (Backlog Free).

Katika ziara yake wilayani hapo alipata fursa ya kutembelea Gereza la Wilaya na kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu. Aidha aliwapongeza wadau wote wa haki jinai kwa kazi nzuri wanayofanya kwani hali ya Gereza ilionesha kuwa ni nzuri na hakuna msongamano.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyeketi mbele) akisaini kitabu cha wageni alipowasili Mahakama ya Wilaya Iramba hivi karibuni. Aliyeketi kulia ni Mhe. Sylvia Lushasi, Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akiwasikiliza kwa Makini watumishi waliokuwa wakijitambulisha  (hawapo pichani). kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylvia Lushasi akisaini kitabu cha wageni.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylvia Lushasi akizungumza na watumishi (hawapo katika picha).

Sehemu ya watumishi wakimsikiliza kwa makini  Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (hayupo katika picha).Wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw Yusuph Kasuka, katikati ni Msaidizi wa Jaji, Mhe. Getrude Misana  na  kulia ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Iramba, Mhe Sydney Nindi.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni