Na Mwinga Mpoli-Mahakama Kuu, Mbeya
Mahakama Mkoa wa Mbeya hivi karibuni iliendesha zoezi
la utoaji elimu kwa Watendaji wa Kata kuhusu mambo muhimu wanayopaswa kuzingatia wanapoandaa barua kwa ajili ya washitakiwa kupata dhamana
mahakamani.
Zoezi hilo lilifanyika katika ukumbi wa mikutano Mahakama
Kuu Mbeya likihusisha Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, baadhi
ya Mahakimu, Mawakili wa Serikali pamoja na Watendaji wa Kata wa jiji la Mbeya.
Akiongea katika ufunguzi wa zoezi hilo, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Tedy Mlimba aliwahimiza Watendaji hao
kuzingatia taratibu za utoaji wa barua za dhamana ili wasiingie kwenye matatizo.
Aliwaomba kuwa na uthibitisho wa mali zinazowekwa
dhamana na wadhamini wawe wanatoka kwenye maeneo yao ya kiutawala ili
kurahisisha upatikanaji woa pindi washtakiwa wanapotoroka au wanaporuka dhamana.
“Tujitahidi kutoa barua za dhamana kwa kuzingatia
sheria, taratibu na kanuni,” alisisitiza Mhe. Tedy.
Naye Wakili wa Serikali Lodgud Eliamani alisisitiza
dhamana ni haki ya kila mtu, hivyo Watendaji wasishiriki katika kuzuia barua za
dhamana. Alitumia nafasi hiyo kuwaelimisha juu ya makosa yenye dhamana na
yasiyo na dhamana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Watendaji hao, Bw. Jumapili
Mwasenga, kwa niaba ya wenzake, alishukuru kwa elimu waliyopata kwani imewawezesha
kufahamu na kujua nini kinapaswa kufanyika.
Aliomba yaandaliwe mafunzo ambayo watapata muda wa
kutosha pamoja na wenyeviti wa mitaa wao ili nao waelewe mambo yanayotakiwa
kufanyika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni