Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Wito umetolewa kwa
wananchi kusema ukweli pindi wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za makosa ya
jinai, hatua itakayosaidia kupunguziwa adhabu.
Wito huu ulitolewa
Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi
alipokua akitoa elimu kwa wananchi waliohudhuria mahakamani hapo.
Mhe. Mkhoi alisema
pengine mtu akiwa ametenda kosa katika mazingira tatanishi anapaswa kusema
kweli wakati wa kujitetea ili Mahakama ione kama alifanya hivyo kwa kukusudia
au bila kukusudia.
“Mfano, mtu
ameokota bastola na akakamatwa nayo, inabidi aseme ukweli pindi ukifika wakati
wa kujitetea ili Mahakama iweze kuona nia yake ya dhati na kufikiria kupunguza
adhabu kwa mhusika,” Mhe. Mkhoi alisema.
Akiendelea kutoa
elimu kuhusu makosa ya uhujumu uchumi, Hakimu Mfawidhi alieleza sheria ya
uhujumu uchumi imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara kutokana na makosa
hayo kuongezeka, hivyo kuongezeka pia adhabu.
Alisema adhabu ya hapo
awali ilikua kulipa faini au kifungo, hivyo watu wengi waliweza kulipa faini na
kuendelea kufanya uharifu tena.
“Kwa sasa adhabu ni
kifungo kisichopungua miaka 20 na kisizozidi miaka 30. Lengo la kuongeza adhabu
ni kuwafanya watu wajifunze na kutofanya makosa haya wakihofia adhabu kali,”
alisema.
Mhe. Mkhoi
amewaomba wananchi kuhudhuria mahakamani hapo ilikupata elimu itakayowasaidia kuepuka
kutenda makosa pasipo kujua kama ni kosa. Aliwakumbusha kuwa kutokujua sheria
sio kinga ya kutokuadhibiwa.
Elimu kwa wananchi hutolewa kila siku ya Jumatatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, hatua inayolenga kutekeleza nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama katika kuongeza imani na kukuza uelewa wao kuhusu shughuli za Mahakama.
Baadhi ya wananchi waliofika katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Pwani wakifuiatilia utoaji wa elimu.
Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akitoa elimu katika kutekeleza Mpango
Mkakati wa Mahakama.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na
Mahakama ya Wilaya Kibaha mahali ambapo Mpango Mkakati wa Mahakama unatekelezwa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni