Na Faustine Kapama na Magreth Kinabo-Mahakama
Akizungumza baada ya
kuupokea ujumbe huo ulioongozwa na Kiongozi wa Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za
Mahakama ya Tanzania kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor, Mtendaji Mkuu
alielezea maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza
jukumu lake la kutoa haki kwa wananchi na kuimarisha miundombinu mbalimbali,
ikiwemo majengo.
Ameuhakikishia ujumbe huo
kuwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili
wa Benki ya Dunia inaendelea vizuri, siyo tu katika majengo yenyewe, lakini pia
matokeo chanya yanayoonekana kutokana na huduma bora zinazotolewa.
Prof. Ole Gabriel alitoa
mfano wa ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, ikiwemo kile cha Masuala ya
Familia Temeke ambacho mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kiasi cha kufikiria watumishi
wa Mahakama kuanza kutoa huduma kwa masaa 24.
Ameuambia ujumbe huo wa
Benki ya Dunia kuwa kila kitu kwa sasa kinaenda vizuri katika mstakabali mzima
wa uendelezaji wa miundombinu mbalimbali na hakuna changamoto kubwa ambayo
wanaweza kuielezea kukwamisha utekelezaji wa miradi inayoendelea.
“Ninavyojua, kila kitu kiko chini ya udhibiti wetu wa ndani, daima kumekuwa
na usaidizi na uungwaji mkono tangu mwanzo. Kwangu hilo ndilo la muhimu zaidi. Daima
mambo huelekea kwenye mwelekeo sahihi kama kuna ushirikiano. Kwa unyenyekevu
mkubwa, naomba tuendelee na kasi hii hii,” alisema.
Mtendaji Mkuu, kwa niaba
ya Jaji Mkuu, alitoa shukrani zake kwa namna timu kutoka Banki ya Dunia
inavyoshirikiana na Mahakama katika kuhakikisha mipango yote inatekelezwa
kikamilifu.
Prof. Ole Gabriel aliwaalika Benki ya Dunia kushiriki katika Mkutano mkubwa wa Majaji Wakuu kutoka nchi zote za Bara la Afrika unaotarajia kufanyika Tanzania kwa mara ya kwanza jijini Arusha mwishoni mwa mwezi Octoba, 2023.
Kiongozi wa jumbe huo
alitumia nafasi hiyo kumtambulisha Mtaalamu Kiongozi wa Utawala kutoka Benki ya
Dunia, Bi. Donna Andrews ambaye anaungana na timu hiyo kufuatilia utekelezaji
wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini.
Bi. Donna alieleza kuwa ingawa
bado ni mgeni lakini ameshasikia maendeleo mazuri ya miradi mbalimbali inayotekelezwa
na Mahakama nchini na kwamba inaeleweka kumekuwepo na mafanikio makubwa.
Alielezea pia furaha yake
kwa kukutana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama na kufanyakazi pamoja na timu hiyo ya
Benki ya Dunia na aliahidi kuendeleza ushirikiano ulipo kati ya pande mbili.
Tukio hilo la utambulisho lilihudhuriwa pia na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha na Mtalaam wa Utawala kutoka Benki ya Dunia, Bw. Benjamin Mtesigwa.
(Picha na Magreth Kinabo-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni