Jumanne, 26 Septemba 2023

ENDELEENI KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO: JAJI KARAYEMAHA

Na. Mwinga Mpoli – Mahakama Mbeya.

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Mbeya wameaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano uliotukuka ili kuleta matokeo chanya katika utendaji wao wa kazi.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni katika hafla fupi ya kuwaaga Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. James Karayemaha aliyehamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea ambapo amepangiwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Projestus Kahyoza ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es salaam.

“Nawashukuru sana kwa msaada na ushirikiano mlionipa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, mafundisho niliyoyapata hapa yamenisaidia sana na watumishi wote kwa ujumla mmekuwa watu wema sana kwangu. Matunda ya kazi na ushirikiano mliokuwa mkinipatia ndiyo haya na hivyo nawaomba muendelee kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano” alisema Mhe Jaji Karayemaha.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mhe. Projestus Kahyoza alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa bidii, kuendelea na mazoezi na zaidi kudumisha mshikamano uliopo baina ya watumishi kwani ndiyo nguzo kubwa ya kuwafikisha kwenye malengo waliyojiwekea.

“Tujitahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano mliokuwa mkinionyesha hata kwa viongozi wanaobaki na watakaokuja, lakini pia msiache mazoezi kwani kazi nzuri na ya uhakika inachangiwa na afya bora” alisisitiza Mhe. Kahyoza

Aidha, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dastan Ndunguru aliwashukuru Mhe. Karayemaha pamoja na Naibu Msajili Mhe. Kahyoza kwa kipindi chote walichofanya kazi pamoja Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya na kuwatakia kila lenye kheri kwenye majukumu yao mapya.

Nao watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya walionyesha kuguswa na tukio hilo, na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kudumisha mshikamano uliopo baina yao na pia kuwapatia viongozi hao zawadi mbalimbali.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. James Karayemaha (kushoto) akiwa ameketi pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Projestus Kahyoza (kulia) wakati wa hafla ya kuagwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. James Karayemaha akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda hiyo (hawapo pichani)


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Projestus Kahyoza akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kuagwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. James Karayemaha (kushoto) akiwa ameketi pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Projestus Kahyoza (kulia) wakipeana mikono kama ishara ya kuagana wakati wa hafla ya kuagwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya.


Sehemu  ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya walioshiriki hafla hiyo.


Sehemu  ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya walioshiriki hafla hiyo.


Sehemu  ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya walioshiriki hafla hiyo.

(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni