Jumanne, 26 Septemba 2023

HUDUMIENI WANANCHI KWA LUGHA ZENYE STAHA; JAJI KULITA

Na Emmanuel Oguda- Mahakama, Shinyanga

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita amewataka watumishi wa Mahakama Wilaya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla kutoa huduma kwa wananchi kwa lugha zenye staha na kwa weledi ili kuwasaidia wananchi ambao idadi kubwa hawana uelewa wa kutosha wa masuala ya Mahakama.

Jaji Kulita aliyasema hayo jana tarehe 25 Septemba, 2023 akiwa katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama Wilaya ya Kishapu ambapo ameeleza kuwa asilimia kubwa ya watumishi wa Mahakama ambao hawakuwa na weledi katika kutekeleza majukumu yao wengi wao hawapo kazini, hivyo, kila mmoja anao wajibu wa kuhakikisha kuwa anatoa huduma bora kwa wananchi kwa lugha zilizo na staha.

“Kila mmoja akitimiza wajibu wake, wananchi watapata huduma zilizo bora na tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa kutoa haki kwa wakati,’’ alisema Jaji Kulita.

Aidha, Mhe. Kulita aliwasisitiza watumishi hao kuwa, wanao wajibu wa kutambua majukumu yao waliyoelekezwa kuyafanya kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za Utumishi wa Umma pamoja na kufuata Kanuni za Uendeshaji wa Mahakama za mwaka 2021. 

Mhe. Kulita pia amewataka watumishi wa Mahakama kutumia fursa za ukaguzi katika kufanya maboresho ya maeneo mbalimbali ya utendaji kazi wa Mahakama, aidha, aliongeza kuwa, kwa sasa Mahakama ya Tanzania ipo katika matumizi ya TEHAMA, hivyo ni vema kila mmoja akashiriki kikamilifu katika kuifanya Mahakama kuwa ya Mtandao.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kishapu, Mhe. Johanitha Rwehabula, amewapongeza watumishi wa Mahakama hiyo kwa ushirikiano na kufanya kazi kwa kujituma licha ya uchache wao.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti aliendelea kuwasisitiza watumishi wote wa Mahakama Mkoa wa Shinyanga kuendelea kuzingatia nidhamu na weledi kama ambavyo wamekuwa wakikumbushana kupitia salaam ya Mahakama ya Tanzania ya Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji.

Mhe. Kulita yupo katika ziara ya kawaida ya ukaguzi wa Mahakama Mkoa wa Shinyanga iliyoanza tarehe 25 Septemba na kumalizika leo tarehe 26 Septemba, 2023 ambapo atatembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mahakama za Wilaya Shinyanga na Kahama.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu (hawapo katika picha) alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama wilayani hapo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu, Mhe. Johanitha Rwehabula akisikiliza kwa makini maelekezo ya Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Kulita alipofanya ziara ya ukaguzi Mahakama ya Wilaya Kishapu.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kishapu wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita (hayupo katika picha) wakati wa ziara yake ya ukaguzi katika Mahakama hiyo.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni