Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe
amekabidhi ofisi kwa Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Latifa Mansoor jana tarehe 25
Septemba, 2023 ikiwa ni baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Mhe.
Mansoor ambaye kabla ya kuja Morogoro alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masjala Kuu Dar es Salaam ambapo akiwa huko alichaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) ngazi ya Tawi la
Mahakama Kuu, Masjala Kuu.
Katika
hafla ya makabidhiano, Majaji hao walipata wasaa wa kuzungumza na watumishi pamoja
na wadau wa Mahakama, ambapo Mhe. Ngwembe alitumia nafasi hiyo kuagana na
wanamorogoro, huku Mhe. Mansoor akatumia wasaa huo kujitambulisha na kuwatambua
watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo.
Akitoa
shukrani wakati wa kuagana na watumishi, Mhe. Ngwembe alisema kuwa ushirikiano
alioupata toka Kanda ya Morogoro usiishe mara baada ya kuondoka kwake bali
uendelee kwa Kiongozi huyo mpya na hata Viongozi wengine watakaoendelea kuja kwenye
Kanda hiyo.
“Leo
ni siku yangu ya pekee na adimu, nalazimika kuagana na watumishi niliokuwa nao
tokea 2021, watumishi hawa wamenipa heshima kubwa sana, Viongozi hawawezi
kufanya kazi peke yao isipokuwa kwa ushirikiano na umoja wetu,” alisema.
Naye
Mhe. Mansoor alipokea kwa mikono miwili makaribisho aliyoyapata kwa watumishi
wa Kanda hiyo, huku akisisitiza kuwa ofisi yake ipo wazi kwa yeyote mwenye
mawazo ya kuboresha. Alisisitiza kuwa yeye ni mtu wa kazi na anavutiwa zaidi na
wachapakazi.
“Nashukuru
kwa uongozi wa Mahakama kwa kuona kuwa mimi naweza kuziba pengo la Mhe. Ngwembe,
nimeona na nimeambiwa mafanikio ya Kanda ya Morogoro, sifa ya Morogoro kutoa
elimu ni utamaduni mzuri nitaomba tuendelee nao,” alisema.
Akitoa
neno la shukrani kwa niaba ya watumishi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata alisema kuwa wataendelea kutoa
ushirikiano kwa Kiongozi wao mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi
mkubwa.
Kauli hiyo iliungwa mkono Jaji mwingine wa Mahakama hiyo, Mhe. Messe Chaba ambaye aliongeza kuwa wapo tayari kuyapokea maelekezo toka kwa Kiongozi huyo na kuonesha ushirikiano.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Paul Ngwembe (kushoto) akimkabidhi taarifa ya Kanda Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (kulia) wakati wa makabidhiano ya ofisi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (kushoto) akipokea zawadi ya ua toka kwa aliyekuwa Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Messe Chaba (kulia) ikiwa ni ishara ya ukaribisho.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (aliyesimama) akizungumza na
wanachama wa TAWJA Kanda ya Morogoro. Picha chini akipokea zawadi toka TAWJA.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (kushoto)
akimlisha keki Mtendaji wa Mahakama Kanda, Bw. Ahmed Ng’eni na kulia ni Naibu Msajili
Mhe. Agustina Mbando.
Sehemu
ya watumishi na wadau wa Mahakama (juu na chini) wakifuatilia hotuba ya Jaji Latifa Mansoor
(hayupo pichani).
Tukio
la makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi toka kwa Mhe. Paul Ngwembe, aliyekaa
mbele kwenda kwa Jaji Mfawidhi mpya wa Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor
(wa pili kulia). Wengine ni Jaji Messe Chaba (wa tatu kushoto), Jaji Gabriel
Malata (wa kwanza kulia), Naibu Msajili, Mhe. Augustina Mmbando (wa pili
kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Ahmed Ng’eni (wa kwanza kushoto).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni