Jumanne, 26 Septemba 2023

MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA YAPATA JAJI MFAWIDHI MPYA

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma imepata Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Augustine Rwizile ambaye anachukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake Mhe. Lameck Mlacha ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Jana tarehe 25 Septemba, 2023, Kaimu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga aliongoza watumishi wa Kanda hiyo kumpokea Mhe. Rwizile aliyewasili kituoni hapo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kuripoti kazini.

Akizungumza na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Lameck Mlacha pamoja na Mhe. Rwizile waliowasili mahakamani hapo kwa pamoja, Mhe. Magoiga aliwaeleza Viongozi hao kuwa, Kituo pamoja na Mahakama zote za Kanda ya Kigoma vipo salama  katika kipindi chote alichokaimu nafasi hiyo ya ufawidhi. 

“Kwa niaba ya watumishi wa Kanda ya Kigoma tunayo furaha kubwa kukupongeza Mhe. Mlacha kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan uendelee kutumikia Taifa katika nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, aidha tunakupongeza pia Jaji Mfawidhi, Mhe. Rwizile na pia tunakukaribisha Kanda ya Kigoma,” alisema Mhe. Magoiga.

Aidha, Mhe. Magoiga alitumia fursa hiyo kubainisha kwamba naye amepata  uhamisho  kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Manyara na hivyo anajipanga kufanya taratibu za makabidhiano ili aweze kuripoti katika kituo chake kipya.

Akimkaribisha Jaji Rwizile katika kituo kipya cha Mahakama Kuu Kigoma, naye Jaji Mlacha alimfahamisha Jaji mfwidhi huyo kuwa, Mkoa wa Kigoma ni mzuri wenye maendeleo makubwa kwa sasa na watumishi wake ni wachapa kazi hivyo ni sehema nzuri na wezeshi kufanyia kazi. 

“Una timu nzuri ya utendaji kazi hivyo itumie vema katika utekelezaji wa Dira ya Mahakama ya utoaji wa haki kwa wakati” alisema Jaji Mlacha.

Mhe. Mlacha aliongeza kwa kumpongeza Mhe. Magoiga kwa kupata uhamisho kwenda kituo kipya cha Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kuwahudumia wananchi waliopo huko huku akimsisitiza kuchapa kazi katika kituo kipya kwakuwa mtumishi wa Umma hachagui kituo.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile aliwashukuru watumishi wa Kanda hiyo kwa mapokezi mazuri na yenye kujaa furaha huku akisema hiyo ni ishara ya kuonesha kuwa Kigoma ni sehemu njema hivyo ataendeleza mazuri aliyoyakuta. 

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akisaini kitabu cha wageni jana tarehe 25 Septemba, 2023 mara baada ya kuwasili katika ofisi yake mpya Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kushoto) akipokea  shada la maua kutoka kwa Bi. Shamsa Abdallah  ikiwa ni ishara ya kumpokea kwa upendo katika Kanda hiyo.

Aliyekuwa Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephen Magoiga (kulia) akimpokea/kuwapokea na kusalimiana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Lameck Mlacha (kushoto) pamoja na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) walipowasili katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Picha ya pamoja ya Viongozi, katikati ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,  Mhe. Lameck Mlacha, wa pili kushoto Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya  Manyara, Mhe. Stephen Magoiga, wa kwanza kulia ni  Naibu Msajili Mahakama  Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (aliyeshika shada ya maua) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Kanda hiyo.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni