·Yafanya mazoezi ya kufa mtu
·Mwenyekiti asema ameridhika
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) inaendelea na mazoezi makali ya mwisho mwisho ili
kujifua kuelekea mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kuanza mwishoni wa mwezi huu wa Septemba, 2023
mkoani Iringa.
Akizungumza katika
viwanja vya mazoezi vilivyoko Shule ya Sheria maeneo ya Mawasilisho jijini Dar
es Salaam, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema kwa sasa wapo tayari
kwa ajili ya mashindano hayo kwani kiwango kinachoonyeshwa na vijana wake
kwenye mazoezi kinaridhisha.
“Nimeridhika, kama mambo
yataendelea kama hivi na kama hakutakuwa na majeruhi yeyote, tunaenda kwenye
mashindano kuzoa kila kitu. Tuna timu nzuri kwenye kila mchezo na ari ya wachezaji
kwenye maeneo yote ipo juu sana. Kwa kweli safari hii mambo ni mazuri sana,”
alisema.
Alieleza kuwa tangu
wanamichezo kutoka mikoani wawasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya
mazoezi ya pamoja wamethihirisha Mahakama Sports itakuwa timu imara kwenye mashindano.
Dede amewahimiza
wachezaji wote kuendelea kujituma kwenye mazoezi kwa dakika hizi za lala salama
na kuzingatia maelekezo ya Mwalimu ili kukamilisha programu yake kabla ya kuelekea
mkoani Iringa kesho tarehe 27 Septemba, 2023 kwenye mashindano hayo.
Michezo ambayo Mahakama
Sports inatarajia kushiriki katika mashindano hayo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake,
Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake
pamoja na Baiskeli.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni