Jumanne, 26 Septemba 2023

‘MIGOGORO YA KIFAMILIA ISIWE CHANZO CHA KUTOOA, KUOLEWA’

Na Amina Said-Mahakama, IJC Temeke

Kwa mujibu ya Tangazo la Serikali Na. 639, 640 na 641 la mwaka 2021, Kituo Jumuishi cha Utoaji wa Haki Temeke kilianzishwa maalum kwa ajili ya kusikiliza na kuamua mashauri ya mirathi, ndoa na talaka.

Ndani ya mashauri haya, kuna migogoro baina ya ndugu kugombea mali za marehemu pamoja na wanandoa kudaiana talaka kutokana na adha mbalimbali wanazokutana nazo kwenye ndoa zao.

Usikilizwaji wa mashauri haya huambatana na huzuni, vilio, maneno ya kejeli, ugomvi na mara nyingine hupelekea baadhi ya wadaawa kuzirai kutokana na mshtuko au hisia walizokuwa nazo kutokana na uamuzi unaotolewa.

Kama binadamu, matatizo haya hayajaawaathiri wadaawa pekee bali pia huweza kuwagusa Mahakimu, Makarani na watumishi wengine katika kituo hiki wanao wahudumia wadaawa kwa namna moja au nyingine.

Lakini pia imeonekana yaweza kuathiri fikra kwa upande wa watumishi, hivyo kusababisha hofu na baadhi kuchukulia huenda maisha ndivyo yalivyo na pengine kughairi kuingia kwenye ndoa kwa wale ambao bado hawajaoa wala kuolewa.

Ili kuepusha mambo yote haya, hivi karibuni Uongozi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke uliandaa mafunzo maalum ya afya ya akili kwa watumish ili kila mmoja aweze kujitengenezea furaha ndani yake, kuondoa mawazo na kutofanya maisha kuwa magumu.

Akitoa mafunzo hayo, Daktari Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili aliwaeleza watumishi mambo manne yanayojenga maisha yenye afya ambayo ni mazoezi ya mara kwa mara, kupunguza msongo wa mawazo, kula kwa afya pamoja na kunywa maji mengi.

Alishauri pia watumishi kuhakikisha wanalinganisha muda wa kazi na pia kutoa nafasi kwa familia na mambo mengine ya kijamii.

Sambamba na hilo, Uongozi wa Kituo uliteua kikosi maalum kilichoundwa na Mahakimu sita, Afisa utumishi na Mhasibu kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya sababu zinazopelekea mashauri ya mirathi kutofungwa kwa wakati. 

Taarifa kuhusu suala hilo iliwasilishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya kwenye Kituo hicho, Mhe. Simon swai, na kubainisha maeneo mbalimbali waliyofanyia utafiti.

Katika utafiti wake, timu hiyo imeshauri Mahakimu na Majaji wanapoteua msimamizi wa mirathi ni muhimu kushauri hatua gani afuate hadi kufunga mirathi na pia kuwaonya wasimamizi na warithi kufika mahakamani ili kuthibitisha mahesabu na mgawanyo wa mali za marehemu.

Utafiti pia umeonyesha kuwa mwamko wa wananchi wa Dar es Salaam katika kufungua mirathi ni mkubwa na kujengwa kwa Kituo hicho kumeongeza kasi ya wananchi katika kufuatilia mirathi ya wapendwa wao.

Mada zingine zilizowasilishwa uandaaji na uhifadhi wa kumbukumbu za kimahakama iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo katika Kituo hicho, Mhe. Nakijwa Kachua pamoja na taarifa ya uhifadhi wa majalada ya mashauri yaliyomalizika iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya kwenye Kituo hicho, Mhe. Sifa Jacob.

Mafunzo hayo yamewezesha watumishi kufahamu zaidi wajibu wao katika kuwahudumia wananchi na pia kupata mwanga kuhusu afya ya akili na nini kifanyike ili kuimarisha afya zao za akili. Watumishi wakapendekeza mafunzo hayo yawe endelevu na yatengewe siku maalumu walau mara tatu kwa mwaka.

Daktari Garvin Kweka (aliyesimama) akiwasilisha mada ya afya ya akili.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Nakijwa Kachua akiwasilisha mada ya uandaaji na uhifadhi kumbukumbu za kimahakama.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na kikosi kazi cha utafiti wa mashauri ya mirathi kutokufungwa kwa wakati. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Asina Omari. Kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Martha Mpaze.

Picha ya pamoja kati ya Meza Kuu na Mahakimu wa Kituo Jumuishi Temeke.

Picha ya pamoja kati ya Meza Kuu na wajumbe wa manejimenti ya Kituo Jumuishi Temeke.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni