Jumanne, 26 Septemba 2023

JAJI KARAYEMAHA AKABIDHIWA MIKOBA MAHAKAMA KANDA YA SONGEA

Na Hasani Haufi- Mahakama Kuu, Songea

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha amekabidhiwa ofisi rasmi na mtangulizi wake, Mhe. Ephery Kisanya ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Dar es salaam.

Hafla hiyo ya makabidhiano ilifanyika jana tarehe 24 Septemba, 2023 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Songea na kushuhudiwa na wajumbe wa menejimenti wa Kanda hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na Mahakama za Wilaya Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Kisanya alianisha mafanikio yaliyopatikana, ukiachilia mbali uwepo wa mashauri machache ya mlundikano ambayo hayatokani na Mahakama moja kwa moja bali wadau wanaoshirikiana nao. Alisema kuwa mafanikio hayo yamechagizwa na kujituma na ushirikiano kutoka kwa watumishi.

“Katika kipindi cha miezi mitatu niliyoongoza hapa Songea tumeweza kufanya kazi kwa pamoja na mmenipa ushirikiano mzuri na hakuna kilichoharibika. Namkabidhi Mhe. Karayemaha Kituo kikiwa salama kwa sababu nyie ndiyo mliyesababisha kikawa salama,” Mhe. Kisanya aliwaambia watumishi hao.

Kadhalika, Jaji Kisanya aliwaasa kutumia muda vizuri wakiwa kazini na kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa weledi na uadilifu, Alisema kuwa ili Taasisi iweze kufikia malengo yake inatemegemea uwajibikaji wa watumishi katika kila kada.

“Kila mmoja wetu ana fursa au nafasi yake katika kuhakikisha kwamba ile shughuli ya Mahakama ya utoaji haki kwa wananchi inafanyika bila kujali wewe ni dereva, mlinzi, karani na hata mhasibu. Kila mmoja kwa nafasi yake anakuwa anashiriki,” alisema.

Jaji Kisanya aliwahimiza watumishi wote kumpa ushirikiano Jaji Mfawidhi mpya kama waliyofanya kwakwe. “Ninapoondoka amekuja Jaji mpya, endelezeni ushirikiano mliokuwa mnanipa na ikiwezekana uwe zaidi yangu kwani yeye ana vitu vyake na mtaviona,” alisema Jaji Kisanya.

Kwa upande wake, Mhe. Karayemaha alimshukuru mtangalizi wake na kumweleza kuwa yote aliyoyaeleza atayatumia kama funguo za kufungulia milango ya Kanda ya Songea, kwani ameyaona mazuri mengi aliyoyafanya kwa muda mfupi. 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (kulia) akipokea nyaraka mbalimbali za ofisi kutoka kwa mtangulizi wake, Mhe. Ephery Kisanya.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akizungumza na watumishi.

Sehemu ya wajumbe wa menejimenti ya Mahakama Kanda ya Songea ikifuatilia zoezi la kukabidhiana ofisi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Songea akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Lilian Rugarabamu.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni