Jumatatu, 25 Septemba 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA YA KAZI WAELIMISHWA JINSI YA KUANDAA WOSIA

Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama, Kazi

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi imeendeleza utamaduni wake wa kutoa mafunzo kwa watumishi na hivi karibuni iliwapatia elimu juu ya uandishi na uandaaji wa wosia.

Mafunzo hayo yalitolewa na Mwanasheria kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bi. Janeth Mandawa.

Bi. Mandawa alianza kwa kueleza majukumu yanayoshughulikiwa na Wakala ikiwemo uandishi na uhifadhi wa wosia, usimamizi wa mirathi pale mwananchi au Mahakama inaIpoteua RITA kusimamia.

Alieleza vile vile kuwa Wakala inasimamia mali zisizo na mwenyewe na mali za mtoto ambaye hajafikisha umri wa miaka 18 na hana ndugu wa kumsimamia.

Kadhalika, Mwanasheria alielezea maana ya wosia kuwa ni tamko analolitoa mtu enzi za uhai wake akielezea namna anavyopenda mali zake zisimamiwe na kugawanywa kwa warithi wake pindi atakapofariki.

Aliendelea kwa kueleza kuwa tamko hilo mtu analitoa akiwa hai na mwenye akili timamu na mtoa wosia hatakiwi kuwa katika hali ya kulazimishwa, kushurutishwa au kutishwa na anatakiwa awe huru na kueleza warithi wake.

Bi. Mandawa alisisitiza kuwa wosia ulio mzuri ni ule unaoonyesha mgawanyo wa mali kwa warithi ili kuondoa mgogoro na mkanganyiko pindi atakapo kuwa hayupo.

Alifafanua umuhimu wa wosia kuwa na tarehe, sahihi na ushuhudiwe na mashahidi wawili, uandikwe kwa karamu isiyofutika na uwe siri kati ya mtoa wosia na mwandishi.

Bi. Mandawa alitaja aina za wosia ambazo ni ule unaotolewa kwa njia ya mdomo na njia ya maandishi. Alisema waandishi wa wosia wanatakiwa kutaja warithi halali. Alisema mtoa wosia hupata nafasi ya kurithisha mtu yeyote anayempenda ambaye kwa sheria asingekuwa mrithi.

Mwanasheria huyo alieleza umuhimu wa kuandaa wosia kuwa unampa mtoa wosia kurithisha mali kwa warithi wake halali na kumpa nafasi ya kurithisha mtu yeyote amtakaye, kumchagua msimamizi wa mirathi yake na kuchagua wapi azikwe.

Akizungumza katika tukio hilo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina alimpongeza mtoa mada kwa uwasilishaji mahili na kumwomba kuhudhuria wakati mwingine na kuwapitisha watumishi katika sheria za uhandishi na usimamizi wa mirathi.

Aliwaasa watumishi wanapoandaa wosia wawe na afya ya mwili na akili na kurithisha mali ambazo ni halali. Jaji Mfawidhi alifafanua pia umuhimu wa kurithisha watoto waliopatikana nje ya ndoa kwa kufuata kifungu cha 36 cha Sheria ya Mtoto ambacho kinatoa wajibu kwa wazazi kurithisha watoto waliozaliwa nje ya ndoa. 

Mafunzo hayo yalihudhuria na Majaji, Naibu Msajili na watumishi. Utaratibu wa utoaji elimu kwa watumishi na wadau wa Mahakama Divisheni ya Kazi umekuwa ukiratibiwa na Kamati ya Elimu ya ndani, ambayo kwa sasa inaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dkt. Modesta Opiyo. Kwa sasa mafunzo yanapatikana kwa njia ya mtandao (Video Conference) kila siku ya Ijumaa saa 1:30 asubuhi. 

Mwanasheria kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bi. Janeth Mandawa akiendesha mafunzo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni