Jumatatu, 25 Septemba 2023

WADAU HAKI JINAI SINGIDA WAIPONGEZA KANDA YA DODOMA KWA VIKAO VINGI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Wadau wa Haki Jinai mkoani Singida wameipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma kwa kufanya vikao vingi vya kusikiliza mashauri ya jinai mkoani humo hivyo wameahidi kujitoa kwa dhati na kutoa ushirikiano ili kuhakikisha vikao vinavyopangwa vinafanikiwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 25 Septemba, 2023 katika kikao cha awali kilichoongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo kwa ajili ya maandalizi ya vikao maalum vya kusikiliza mashauri ya jinai (criminal session) mkoani Singida.

Katika taarifa ya ufunguzi iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe Sylivia Lushasi amesema jumla ya mashauri 13 ya jinai yanategemewa kushughulikiwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo hadi tarehe 23 Oktoba, 2023.

“Sambamba na taarifa hii, Mkoa wa Singida una mashauri 22 ambayo yanasubiri kusikilizwa (uncauselisted) ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida kuna mashauri 15, Iramba 01 na Manyoni 06,” amesema Mhe. Lushasi.

Mhe. Lushasi amebainisha kuwa mashauri tajwa hayahusishi mashauri yanayosubiri washtakiwa kusomewa kwa mara ya kwanza (plea taking). 

Aidha; Naibu Msajili huyo amewashukuru wadau kwa ushirikiano wanaouonesha na kuomba mshikamano huo uendelee.

Naye Mhe. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amewapongeza wadau kwa ushirikiano ambao wameuonesha katika kufanikisha usikilizwaji wa mashauri hayo na kuwasisitiza Mawakili kunyumbulika (flexibility), kusoma majalada vizuri na kuongea na wateja wao vizuri.

Vilevile, Jaji Mfawidhi ameisisitiza Ofisi ya Mashtaka kuhakikisha malipo ya wasambaza wito yawe yanafanyika mapema ili zoezi la usikilizwaji mashauri lisikwame.

Hiki ni kikao cha nne kwa mwaka 2023 katika kikao hiki Wadau kwa pamoja wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyesimama mbele) akizungumza na wajumbe wa kikao cha maandalizi ya vikao maalum vya kusikiliza mashauri ya jinai (criminal session) mkoani Singida. Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 25 Septemba, 2023.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi (aliyesimama) akisoma taarifa mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt. Juliana Masabo (aliyeketi katikati) pamoja na wajumbe wengine wa kikao hicho. Kulia kwa Jaji Mfawidhi ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida,  Mhe. Allu Nzowa.

Wakili wa Serikali, Bw. Godfrey Songoro (aliyesimama) akisisitiza jambo katika kikao hicho.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Singida, SSP Johannes akisoma taarifa fupi katika kikao hicho.

Wakili wa Kujitegemea, Cosmas Luambano (aliyesimama upande wa kulia) akichangia jambo katika kikao hicho.

Wadau kutoka Magereza wakitoa salaam kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Masabo ( hayupo katika picha).

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni