Na Stanslaus Makendi – Mahakama Kuu Dodoma
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
Dodoma hivi karibuni walipatiwa elimu ya uwekezaji kwenye dhamana za Serikali ili
kuwajengea uelewa namna wanavyoweza kunufaika na uwekezaji huo.
Elimu hiyo ilitolewa na mwezeshaji kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Dar es Salaam, Bw. Fidelis Mkatte ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa ndani wa
utoaji wa elimu kwa watumishi unaoratibiwa na Kamati ya Elimu ya Mkoa.
Katika mafunzo hayo, mwezeshaji aliwaasa washiriki wa mafunzo hayo
kuanza kuwekeza fedha zao katika masoko ya fedha ili waweze kunufaika na huduma
mbalimbali zinazopatikana.
Alisisitiza kuwa uwekezaji huo ni fursa kwa wananchi wote na huiwezesha
Serikali kupata fedha za kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini,
kugharamikia upungufu katika bajeti na faida nyingine lukuki.
Bw. Mkatte alieleza kuwa uwekezaji huo ni salama kwani Serikali
haitarajiwi kukiuka mategemeo ya wadai wake wakati wa malipo unapofika na siyo rahisi
kufilisika kama ilivyo Taasisi nyingine za kifedha na uwekezaj.
“Dhamana za Serikali zinatumika kama dhamana ya mikopo katika Taasisi za
kifedha, zinaweza kuhamishika au kuuzwa na mwekezaji kabla ya muda wake wa
kuiva iwapo atakutana na hali inayomlazimu kufikia uamuzi huo,” alisema.
Alibainisha kuwa BoT, kwa niaba ya Serikali zote mbili yaani Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, huuza
dhamana za Serikali ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka kwa Taasisi mbalimbali
na mwananchi mmoja mmoja.
Bw. Mkatte alisema dhamana za Serikali za muda mrefu ambazo huiva katika
muda unaozidi mwaka mmoja huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani
kupitia minada na baadaye kwenye soko la upili.
“Mtu yeyote au kikundi kilichosajiliwa kinaweza kuwekeza katika dhamana
za Serikali kwani kiwango cha chini cha kuwekeza kwenye dhamana hizo za muda
mrefu ni rafiki kwa kuwa uwekezaji huo huanzia kiwango cha shilingi milioni
moja,” alisema.
Alieleza kuwa utaratibu wa ununuzi na uuzaji wa dhamana hizo hutolewa
kupitia kwenye magazeti na pia taarifa zaidi hupatikana kwenye tovuti ya Benki
Kuu ya Tanzania inayoonyesha itakavyotolewa na tarehe ya mnada.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Dkt. Juliana Masabo, akizungumza wakati wa zoezi hilo alisema mafunzo hayo yamekuwa yenye manufaa kwetu.
“Natamani elimu hii tungeipata mapema zaidi.
Hata hivyo, bado hatujachelewa sana, ni wakati wa kujitafakari na kufanya
maamuzi. Wapo watu tunaowafahamu ambao wamenufaika na
uwekezaji katika dhamana za Serikali,” alisema.
Mhe. Dkt. Masabo aliwashukuru wajumbe wa Kamati ya Elimu inayoongozwa na
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi kwa
kushirikiana na Mtendaji wa Mahakama Kanda, Bw. Sumera Manoti, kwa uratibu
mzuri wa masuala ya utoaji wa elimu kwa umma na watumishi.
Sambamba na hilo, Jaji Mfawidhi aliushukuru uongozi wa BOT kwa kukubali
ombi la kupatiwa mwezeshaji kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo kwa watumishi.
Sanjari na zoezi hilo, watumishi wa Kituo hicho walipatiwa pia elimu
kuhusu mafao ya hitimisho la ajira na mafao mengine yanayotolewa na Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii (PSSSF).
Watumishi hao mwezi ujao wa Oktoba watapatiwa elimu ya mabadiliko ya
kifikra, masuala ya saikolojia na afya ya akili ili kuwajengea uwezo wa
kutekeleza majukumu yao na kumudu maisha yao nje ya kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (wa kwanza kushoto) akimsikiliza mwezeshaji (hayupo pichani) wakati akishukuru kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania kufuatia salam za pongezi na shukrani zilizotolewa na Kiongozi huyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni