Christopher Msagati - Manyara
Mahakimu
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara wameshiriki mafunzo ya siku moja ya
kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutekeleza na kuimarisha jukumu lao la utoaji
haki kwa wote na kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya ndani ya Kanda hiyo.
Akizungumza
katika mafunzo hayo yaliyofanyika jana tarehe 22 Septemba, 2023 mjini Babati
mkoani Manyara, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe.
John Kahyoza aliwakumbusha Mahakimu hao kuyatumia mafunzo hayo kama sehemu
muhimu ya kusaidia kujenga uelewa wa pamoja wa miongozo na taratibu
zinazosimamia jukumu lao la kila siku la utoaji haki kwa wananchi.
“Ni
nafasi muafaka ya kuwekana sawa na kukumbushana yale ambayo tunayafanya kila
siku katika majukumu yetu, na pale ambapo tunaonekana tunafanya kwa kiwango cha
chini, mafunzo haya yatatusaidia kutuimarisha zaidi katika weledi na ufanisi
wetu”, aliongeza Mhe. Kahyoza
Mafunzo
hayo yaliwahusisha Mahakimu wote kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Manyara
inajumuisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara pamoja na Mahakama zake za Wilaya
ambazo ni Babati, Hanang, Mbulu, Kiteto na Simanjiro. Aidha, Mahakimu wa
Mahakama za Mwanzo kutoka Wilaya hizo nao walishiriki mafunzo hayo.
Aidha,
Mada mbalimbali ziliwasilishwa kwa umahiri mkubwa kutoka kwa wawezeshaji wa
mafunzo hayo, ikiwa ni pamoja na Wajibu wa Mahakama katika Kupambana na Rushwa,
Maadili ya Watumishi wa Mahakama, Taratibu za Uendeshaji wa Mshauri mbalimbali
kama vile Uhujumu Uchumi, Ubakaji, Mirathi pamoja na Mshauri yanayosikilizwa
katika Mahakama za Mwanzo. Vile vile Mahakimu hao, walijifunza namna bora ya uandaaji
wa Bajeti pamoja na utekelezaji wake.
Kwa
upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. Benard
Mpepo aliwakumbusha Mahakimu hao juu ya utekelezaji wa maagizo ya Nyaraka
mbalimbali zinazotolewa na Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na Msajili Mkuu.
Imekuwa
ni desturi kwa Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kutoa elimu kwa
watumishi wake mara kwa mara ili kuwaimarisha katika utendaji wa majukumu yao
ya kila siku. Hii ni pamoja na kuwakumbusha kuhusu Maadili.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akitoa
mafunzo kuhusu taratibu mbalimbali za uendeshaji wa mashauri kwa Mahakimu (hawapo pichani) jana tarehe 22 Septemba, 2023 mjini Babati mkoani Manyara.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo akifafanua kuhusu
Nyaraka mbalimbali zinazotoka kwa Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na Msajili Mkuu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu walioshiriki mafunzo hayo. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. Gladys Barthy (wa pili kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Bernard Mpepo (wa kwanza kushoto) na wa pili kulia ni Afisa kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara Bw. Sadiki Nombo.
(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
H
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni