Jumanne, 12 Septemba 2023

HAKIMU KIBAHA AWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU KUBAMBIKIWA KESI

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona amewatoa hofu wananchi kuhusu suala zima la kubambikiwa  mashauri maana mashauri hayo yakifika mahakamani ukweli hubainika. 

Akizungumza na wananchi hao waliofika kupata huduma katika Mahakama hiyo jana tarehe 11 Septemba, 2023 alipokuwa akitoa elimu katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Kibona amesema kesi za kutengeneza zinajulikana mapema  zikifika mbele ya Mahakama.

“Huwezi kuthibitisha kesi ya kutengeneza kwa kuwapanga mashahidi watano wote waseme uongo unaofanana lazima watajichanganya tu” alisema Mhe. Kibona.

Alisema tofauti iliyopo kati ya mashauri ya madai yanaangaliwa mizani uzito ulipo lakini kwa kesi za jinai zinatakiwa kuthibitishwa pasipo kuacha shaka na pia katika kesi za jinai lazima kuwepo na nia ovu ya kutenda kosa hilo.

Amewatoa shaka wananchi hao kuwa hisia haziwezi kusasabisha mtu kutiwa hatiani isipokua ushahidi uliothibitika pasi na kuacha shaka ndio utamtia mtu hatiani. 

Akifundisha kwa mifano Mhe. Kibona ametoa mfano mmoja wa ng’ombe aliyekuwa amefungwa kamba na mfugaji, ng’ombe huyo akikata kamba na kwenda kwenye shamba na kuharibu mazao hiyo haiwezi kuwa jinai kwa sababu hakuna nia ovu maana yeye alimfunga na ng’ombe ndiye aliyekata kamba na kwenda kuharibu mazao bila mfugaji kujua. 

Aliongeza kuwa, katika tukio kama hilo, haiwezi kuwa kesi ya jinai maana hakuna nia ovu ya mfugaji kuruhusu ng’ombe wake kwenda kuharibu mazao. Hivyo katika kisa hicho aliyeharibiwa mazao anapaswa kufungua kesi ya madai badala ya jinai.

Aliendelea kufafanua zaidi, ambapo alitoa mfano wa shauri halisi lililotokea zamani na imeandikwa katika vitabu vya mkusanyiko wa mashauri, shauri la Chacha Mginga, Mhe. Kibona alisema katika kesi hiyo Mahakama ilimuhukumu mshtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, maana ndani ya mshtakiwa hakukua na nia ovu ya kuua.  

Kwa mujibu wa Mhe. Kibona, mshtakiwa alikuwa anawinda nyani wasiharibu mazao yake akakuta watu wawili usiku shambani wakifanya mapenzi kwa kuwa ilikua usiku ilibidi aulize kama ni watu au la, aliuliza mara tatu hakukuwa na jibu kwa mawazo yake alitarajia kama ni watu watajibu kwa kukaa kimya alijua sio watu bali ni nyani hivyo alifyatulia mshale ambao ulimuua mmoja na hivyo alishtakiwa na kosa la mauaji ya kukusudia lakini kutokana na ushahidi ilionekana aliua bila kukusudia.

Akijibu swali lililoulizwa na mwananchi ambaye jina lake hakutaka litajwe kuhusu kumhisi mtu kumbambikia kesi, Mhe. Kibona alieleza kuwa hisia haziwezi kumtia mtu hatiani isipokua ushahidi uliothibitika bila kuacha shaka ndio utamtia mtu hatiani.

Aidha, Mhe. Kibona aliongeza kuwa, sio kwamba Hakimu hufurahia kusoma hukumu ya kumfunga mtu, Hakimu naye ni binadamu hivyo anajisikia vibaya wakati mwingine kumfunga mtu lakini anajisikia vizuri pia kwa kutimiza wajibu wake wa kutoa haki bila kupendelea upande wowote.

Alieleza kuwa, Mahakama imebeba asilimia 50 za upande wa mshtakiwa na asilimia 50 za upande wa mashtaka hivyo amekaa pale kama muamuzi kwa yule atakayethibitisha au kutengua mashtaka yeye atatoa maamuzi akizingatia ushahidi na sheria inasemaje.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani wakipata elimu ya Mahakama kutoka kwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona (hayupo katika picha).

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona akitoa elimu kwa wananchi (hawapo katika picha) waliofika kupata huduma katika Mahakama hiyo.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni