Jumanne, 12 Septemba 2023

IJA YAENDESHA MAFUNZO KWA MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA, UADILIFU WASISITIZWA


Na Mwandishi wetu.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Ndoa na Mirathi, Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa amefungua mafunzo ya wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama, na kuwataka washiriki kuwa waadilifu watakapopata sifa na watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao, ili kuhakikisha haki inatekelezwa vema kwa pande zote mbili, ya mteja wanayemuhudumia na mtoa haki ambaye ni Mahakama.

 

Mhe. Jaji Mwanabaraka amefungua mafunzo hayo  tarehe 11 Septemba, 2023, katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), jijini Dar es Salaam ambayo yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na yanatarajia kufanyika hadi tarehe 25/09/2023.

 

Chuo cha IJA kinaendesha mafunzo haya kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na ya 6 za Kanuni za Madalali  na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Tangazo la Serikali Na.363 za mwaka 2017.

 

"Kazi ya usambazaji nyaraka za Mahakama inahitaji uadilifu wa kiwango cha juu, uadilifu kwa mteja unayemhudumia, lakini pia uadilifu kwa sisi ambao mwisho wa siku ndio utatusaidia kwenye kutoa haki, utakaposema mteja hakupatikana wakati hukumtafuta, tayari utakuwa hujatenda uadilifu na unaweza kusababisha haki isitendeke ipasavyo," amesema Mhe. Mwanabaraka.

 

Pia Mhe. Jaji Mwanabaraka amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya maboresho makubwa ya Mahakama yanayolenga kuondoa malalamiko ya wananchi waliyokuwa kuhusu ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watu wanaojishughulisha na kazi hiyo ya udalali  na usambazaji wa nyaraka za Mahakama.

 

"Mafunzo haya ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea katika mhimili wa Mahakama kwa lengo la kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi hususani suala la ukosefu wa uadilifu na uelewa sahihi wakati wa utekelezaji wa majukumu ya udalali na usambazaji wa nyaraka za Mahakama," amesisitiza.

 

Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo haya, Bw. Nuhu Mtekele kutoka IJA, amesema kuwa mafunzo hayo yana malengo makubwa matatu, ikiwemo kuwawezesha washiriki kupata uweledi juu ya kazi hiyo na pia kuunga mkono juhudi za Serikali za kuweza kutoa ajira.

 

"Mafunzo haya yana malengo makubwa matatu, kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama ili kuwawezesha madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama kuweza kufanya kazi hiyo kwa uweledi, pili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuweza kutoa ajira, kwa kuwa washiriki wakitoka hapa wanakwenda kujiajiri au kuajiriwa, hivyo unakuwa ni mchango mkuwa wa IJA kuongeza wigo wa ajira nchini," amesema Mtekele.

 

Aidha Mratibu huyo ameongeza kuwa, "Mwisho mafunzo haya yanasaidia ukuaji wa sekta binafsi, kwani madalali wa Mahakama pia wanakuwa na sifa ya kutumika na taasisi mbalimbali kama mabenki katika kufanya kazi ya upigaji minada, hivyo kama benki zitahitaji kukusanya madeni, zikiwatumia watu hawa ambao wamepatiwa mafunzo haya, maana yake watakuwa wanawatumia watu wenye uweledi mkubwa,” amesisitiza

 

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo haya, akiwemo Bw. Boaz Ackimu Boaz kutoka kampuni ya udalali ya Isoko Auctioneers & Court Broker amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani ni kazi nyeti inayohitaji uadilifu mkubwa.

 

"Kama washiriki tunategemea kujifunza maadili yanayoongoza tasnia hiii ya udalali wa Mahakama na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama. Ifahamike kuwa hii ni kazi nyeti inayohitaji uadilifu mkubwa, hivyo ni muhimu kwetu kujifunza sheria na kanuni zinazoongoza tasnia hii," amesema Bw. Boaz.

 

Mshiriki mwingine, Bi. Aneth Ndimuhela kutoka kampuni ya Rapitech Solutions Ltd ametaja faida zingine watakazozipata kupitia mafunzo hayo.

 

"Haya mafunzo yana mchango mkubwa kwetu kwani yanatusaidia kuongeza ujuzi na kuweza kufanya kazi kwa uweledi na kupata sifa stahiki za kufanya kazi hii. Pia kama ilivyo kawaida, sisi tunatakiwa tutende haki kwa mteja aliyetupa kazi na yule tunayemwendea ndio maana tunapatiwa mafunzo haya," amebainisha Ndimuhela.

Jaji wa Mahakama Kuu  ya Tanzania, ambaye pia ni Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia ,Temeke Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, akihutubia wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wenye nia ya kufanya kaz,i ya udalali na usambazaji wa nyaraka za Mahakama.Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) na yanafanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), mkoani Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Pamela Majengo akiwasilisha mada wakati  wa mafunzo  hayo.

Washiriki wa mafunzo  hayo wakifuatilia mada kutoka kwa mwezeshaji(hayupo pichani). 

Mshiriki Aneth Ndimuhela akichangia jambo Washiriki wa mafunzo ya wenye nia ya kufanya kazi ya udalali na usambazaji wa nyaraka za Mahakama yanayofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), mkoani Dar es Salaam.

Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Temeke Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki ya mafunzo ya wenye nia ya kufanya kazi ya udalali na usambazaji wa nyaraka za Mahakama.Kushoto ni mratibu wa mafunzo hayo, Bw. Nuhu Mtekele kutoka IJA na kulia ni Mhe. Pamela Mazengo, Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama) 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni