Jumatatu, 11 Septemba 2023

MAHAKAMA ‘FC’ YAICHAPA SHYTOWN VETERANI BAO MOJA KWA NUNGE

Emmanuel oguda, Mahakama Shinyanga

Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Mahakama FC imeichakaza timu ya wakongwe wa mpira ya mkoani humo ‘Shytown Veteran’ kwa bao 1 kwa nunge. 

Mtanange huo wa kirafiki umepigwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kom iliyopo Manispaa ya Shinyanga, bao hilo liliwekwa wavuni na mshambuliaji wa Mahakama FC Patrick Mluge dakika ya 43 ya kipindi cha kwanza. 

Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, timu ya Shytown Veterani ilianza mchezo kwa kasi kubwa huku ikiwatia presha Mahakama FC ambao awali walionekana kutosomana vyema, mashambulizi zaidi yalielekezwa katika lango la Mahakama FC ambapo hata hivyo mikwaju hiyo ilikuwa ikidhibitiwa vilivyo na mlinda mlango wa Mahakama FC Novat Mgongolwa. 

Dakika ya 20 ya kipindi cha kwanza Mahakama FC walionekana kuanza kusomana vyema kwani tayari walikuwa wamewasoma vilivyo wapinzani wao.

Mahakama FC iliendeleza mashambulizi zaidi kwa lango la Shytown ‘Veteran’ ambapo mashuti kadhaa yalielekezwa kwenye lango la wapinzani kupitia mshambulizi machachari wa Mahakama FC Patrick Mluge.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika, Mahakama FC ilikuwa inaongoza kwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Shytown Veterani.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Mahakama FC ilifanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji ambapo Mohamed Kibula na Gustaph Awonda waliingia kuongeza mashambulizi zaidi wakichukua nafasi za Patrick Mluge na Michael Turuka. 

Mashambulizi zaidi yalielekezwa Zaidi kwa Shytown Veterani ambao walionekana kuelemea na mashambulizi kutoka kwa vijana wa Mahakama FC.

Hadi dakika 90 za mchezo zinakamilika, Mahakama FC waliibuka washidi kwa bao 1 – 0 dhidi ya Shytown Veterani.

Akizungumza baada ya mchezo kukamilika, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Frank Mahimbali ambaye alishuhudia mtanange huo, aliwapongeza wachezaji wa Mahakama FC kwa ushindi dhidi ya Shytown Veterani. 

“Niwapongeze sana kwa ushindi wa leo, ni hatua kubwa toka tumeanza mazoezi na tunaonekana kuimarika zaidi, sasa tuendelee na mazoezi ya kutafuta pumzi pamoja na stamina ili tuweze kuimarika vizuri zaidi,’’ alisema Mhe. Mahimbali.

Kwa upande wake Msemaji wa Shytown Veteran Seif Wamkote alisema, “michezo ni afya, michezo inaimarisha mahusiano na niwapongeze Mahakama FC kwa kutualika kwenye mechi hii ya kirafiki, ninaomba michezo hii iwe endelevu ili tuzidi kuimarisha mahusiano pamoja na afya kwa ujumla.’’ 

Mahakama FC inaendelea na maandalizi kuelekea Bonanza kubwa la michezo linalotarajia kufanyika mwezi Novemba, 2023 litakalofanyika mjini Bukoba, likihusisha Kanda 5 za Mahakama Kuu za Bukoba, Musoma, Mwanza Shinyanga na Tabora.

Kikosi cha mpira wa miguu cha Mahakama FC ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kikiwa katika picha ya pamoja katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kom Shinyanga.

Kikosi cha mpira wa miguu Shytown 'Veteran' ya Mjini Shinyanga katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo dhidi ya Mahakama FC.

Mpambano ukiendelea kati ya Kikosi cha mpira wa miguu cha Mahakama FC ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga na Kikosi cha mpira wa miguu Shytown 'Veteran' ya Mjini Shinyanga katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kom Shinyanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza na wachezaji wa Mahakama FC mara baada ya 
kumalizika kwa mchezo dhidi ya Kikosi cha mpira wa miguu Shytown 'Veteran' ya Mjini Shinyanga.

Msemaji wa Shytown Veterani Seif Wamkote akizungumza jambo mara baada ya mchezo kukamilika.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni