Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania
imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baada ya kukukutana na Sekretariet ya
Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Zanzibar kwa lengo la kufahamiana na
kubadilishana uzoefu wa kazi katika masuala ya utoaji haki.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na
watumishi wa Sekretariet hiyo wako katika ziara ya siku mbili visiwani humo
itakayomalizika leo Septemba 12, mwaka 2023.
Akifungua Mkutano baina ya Tume hizo mbili jana Zanzibar,
Prof. Ole Gabriel amewataka watumishi wa Sekretariet hizo zote mbili
kujadiliana kwa kina kuhusu mambo manne ambayo ni muundo wa Tume hizo, nidhamu
na maadili, matumizi ya Teknolojia katika utoaji haki na kuongeza imani ya
wananchi kwa mhimili wa Mahakama.
Alisema ni muhimu wajumbe hao kujadili kuhusu muundo wa
Tume kwa pande zote mbili za Muungano ili kuona mchango wake katika masuala ya
utoaji haki. Aliongeza kuwa japokuwa
kuna tofauti ya muundo wa Tume kati ya Tanzania bara na Zanzibar lakini haki ni
jambo linalogusa watu wote.
Katibu huyo wa Tume pia amewataka wajumbe wa Mkutano huo
kujadiliana namna ya kushirikiana katika matumizi ya Teknolojia ya habari na mawasiliano
kwenye shughuli za utoaji. Alisema
Mahakama ya Tanzania hivi sasa imepiga hatua kubwa kwenye matumizi hayo ambapo
inayo mifumo mbalimbali ya kurahisisha kazi ya utoaji haki.
Aidha Prof. Ole Gabriel alitoa wito kwa watumishi wa
Sekretaet zote mbili za Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa na nidhamu ya hali ya
juu wanapotekeleza majukumu yao ili kujenga taswira chanya ya Mahakama kwa
wadau wake.
”Nidhamu ni jambo la msingi na muhimu kwa watumishi wa
Mahakama kwani bila nidhamu kwa watumishi wa Mhimili huo ni vigumu kwa wananchi
kuwa na imani na Mahakama, pia inarahiusisha mnyororo wa utoaji haki”, alisema
Katibu wa Tume.
Aliwataka watumishi hao wa Tume kulinda taswira nzuri ya
Mhimili wa Mahakama iliyojengeka ili wananchi wawe na imani zaidi na mhimili
huo ambapo alisema tathmini iliyofanyika hivi karibuni inaonesha kuwa kiwango
cha imani ya wananchi kwa Mahakama kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2015
na kufikia asilimia 88 mwaka huu wa 2023.
Kwa upande wake, Katibu wa Tume hiyo kwa upande wa
Zanzibar ambaye pia ni Naibu Mrajis Mhe. Salim Hassan Bakari alisema Mkutano
huo baina ya Tume hizo mbili ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Zanzibar Mhe.
Dkt. Hussein Mwinyi aambapo alizitaka taasisi za Serikali kwa pande zote mbili
za Muungano kushirikiana katika kuwahudumia wananchi.
Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania imeundwa na Ibara
ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha,
majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa
pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka
2011. Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la
kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof.
Elisante Ole Gabriel (Katikati) akizungumza wakati akifungua Mkutano kati ya
Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania Bara na Sekretariet ya
Tume ya Utumishi wa Mahkama Zanzibar leo Visiwani humo. Sekretaerti ya Tume
imeanza ziara ya siku mbili Zanzibar yenye lengo la Kubadilishana uzoefu katika
masuala ya utoaji haki. Kushoto ni Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe. Valentina Katema na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama
Kuu Zanzibar Bw. Kai Bashiru Mbarouk.
Jaji
Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania
Bara na ile ya Zanzibar wakati walipomtembelea ofisini kwake leo ikiwa ni
sehemu ya ziara yao visiwani humo yenye lengo la kubadilishana uzoefu katika
masuala ya utoaji haki kati ya Tume hizo mbili.
Viongozi
wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahkama Zanzibar
wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama
Tanzania Bara leo visiwani Zanzibar.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Sekretariet za Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania Bara na ile ya Zanzibar leo visiwani humo.
Baadhi
ya watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania Bara pamoja na Mahakama
ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Sekretariet ya Tume ya Utumishi
wa Mahkama Zanzibar uliofanyika visiwani humo.
Naibu
Makatibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania Bara na Katibu wa Tume hiyo
Zanzibar wakifuatilia jambo wakati wa Mkutano kati ya Tume hizo mbili. Kulia ni
Naibu Katibu (Ajira na Uteuzi) Bibi Enziel Mtei na kushoto ni Naibu Katibu
(Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya., Katikati ni Naibu Mrajis Mahkama Kuu
Zanzibar ambaye pia ni Katibu wa Tume Mhe. Salum Hassan Bakari.
Baadhi
ya watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania Bara pamoja na Mahakama
ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Sekretariet ya Tume ya Utumishi
wa Mahkama Zanzibar uliofanyika visiwani humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni