Na Abdallah Salum-Mahakama, Njombe
Hakimu
Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama amewahimiza
Mahakimu katika Mahakama za Wilaya mkoani hapa kuendelea na mpango mkakati wa
kumaliza kwa wakati mashauri yanayokaribia kuwa mlundikano kwa kuvuka mwaka toka
yaanze kusikikizwa.
Mhe.
Chamshama alitoa wito huo hivi karibuni kwenye kikao na kusisitiza ifikapo
tarehe 31 Desemba, 2023, Mahakama za Wilaya za Mkoa wa Njombe ziwe zimemaliza aina
hiyo ya mashauri. “Hakikisheni kesi inayoanza kufunguliwa ndiyo inayoanza
kuisha, lengo kuu hapa ni kuondokana na mlundikando,” alisema.
Kadhalika,
Hakimu Mfawidhi aliwasihi watumishi wa Mahakama katika Mkoa huo kuwa na ubunifu
ambao utasaidia utekelezaji wa majukumu ya kimahakama na kuongeza ufanisi. Akahimiza
pia kwenda na mabadiliko ya teknolojia na kutumia mifumo iliyopo, kama JSD2 na
ofisi mtandao (e-office) ili kurahisisha utendaji.
“Mtumishi
yoyote ambaye anaubunifu wa nini kifanyike kwenye utendaji kazi wa Mahakama kwa
hapa Njombe asisite kuusema au kutoa wazo ambalo litasaidia katika utekelezaji
wa misingi ya kimahakama ili kutoa haki kwa wakati na kwa kila mwananchi,”
alisema.
Mhe. Chamshama pia aliwataka watumishi katika
eneo lake kujua haki zao za msingi, ikiwemo stahiki za likizo na maslahi kwa
upana zaidi ili kuondokana na malalamiko ya kiutumishi ya mara kwa mara.
Akizungumza
katika Mkutano huo, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Yusuph
Msawanga aliwahasa watumishi wa Mahakama hiyo kufanya kazi kwa bidii na weledi na
kujituma katika kazi ili kukidhi mahitaji na matarajio ya mwananchi.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Njombe wakiwa kwenye kikao.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni