Alhamisi, 14 Septemba 2023

NENDENI MKATENDE HAKI :RAIS SAMIA

Na Mary Gwera na Magreth Kinabo, Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa haki kwa wananchi bila upendeleo.

Akizungumza na Majaji hao leo tarehe 14 Septemba, 2023 baada ya kuwaapisha Ikulu jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Samia amesema wananchi wana matumaini na Mhimili ,hivyo waende kuongeza imani ya chombo hicho.

“Nawaomba Majaji mlioteuliwa mkaongeze imani kwa wananchi, hakikisheni mnasimamia haki nendeni mkatoe haki kwa wananchi ili mwenye kupata haki apate haki yake anayostahili, msiende kupindisha sheria kwa kuchukua fedha za rushwa mkapindisha haki,” amesema Rais Samia.

Aidha, amesema kwamba, ana imani na Majaji hao ya kuwa, watafanya kazi kwa jitihada na kusaidia kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.

Akizungumzia idadi wa Majaji wa Kuu aliowateua, Mhe. Dkt. Samia amesema ataendelea kuongeza idadi yao kulingana na hali ya uchumi itavyoimarika.

“Katika orodha ya Majaji niliyopatiwa ilikuwa na jumla ya Majaji wa Mahakama Kuu 70, lakini nimeona nianze na Majaji 20 wengine watafuata kadri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu,” ameeleza Rais Samia.

Kuhusu idadi ya Majaji wanawake, Mhe. Dkt. Samia ameeleza kuwa kwa ameteua Majaji saba pekee ingawa alitaka idadi yao iwe 10 kwa 10 kwa kila jinsia, ila ameahidi kwa wakati ujao ataongeza idadi yao.

Kadhalika, Rais Samia ameipongeza Mahakama kwa kuendelea kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi ambao wanakiuka maadili.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kwamba, Mahakama ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wake wanaokiuka maadili.

“Kwa mwaka 2015 hadi 2019, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilipokea jumla ya mashauri 99 ya masuala ya nidhamu, kati ya mashauri hayo watumishi wa Mahakama 33 sawa na asilimia 71 walifukuzwa kazi, waliostaafishwa kwa manufaa ya umma ni 38, waliopewa onyo ni 13 na waliorejeshwa kazini ni 15,” amesema Jaji Mkuu.

Naye, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amempongeza Rais Samia kwa maboresho anayofanya katika Mihimili yote ya Dola ikiwemo Mahakama.

“Napenda kutoka pongezi kwako Mhe. kwa maboresho makubwa unayoendelea kufanya. Kwenu Majaji, Watanzania wana matarajio makubwa kwenu hivyo nendeni mkafanye kazi kwa weledi na uaminifu,” amesema Mhe. Majaliwa.

Kadhalika, Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa rai kwa Majaji hao kutatua changamoto za wananchi.

Uapisho wa Majaji hawa unaongeza idadi yao na kuwa na jumla ya Majaji 30 wa Mahakama ya Rufani na 105 wa Mahakama Kuu ya Tanzania.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa katika picha pamoja na Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania (waliosimama ambao wamevaa majoho), wa tatu kushoto ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, wa pili kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa tatu kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, wa kwanza kulia ni Mhe. Sivangilwa Mwangesi, Kamishna wa Maadili, wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Dkt. Moses Kusiluka. Waliosimama mstari wa mbele (waliovaa suti) wa (pili kulia) ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana, (wa pili kushoto) ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, (kulia kwa Jaji Kiongozi) ni Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na (kushoto kwa Waziri wa Katiba na Sheria )ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo.
Majaji  wakiapa kiapo cha Maadili ya Viongozi wa Umma.
Baadhi ya Majaji na Viongozi 
wengine wa Serikali wakiapa kiapo cha Maadili ya Viongozi wa Umma.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Abdul-Hakim Ameir  Issa akiapa leo ikulu.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Lameck Mlacha akipa leo ikulu.

Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Paul Ngwembe akiapa leo.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.Mustafa Kambona akiapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba yake.

  

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis  Juma akitoa hotuba yake.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, akizungumza jambo kwenye hafla hiyo.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani,akiwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu.

Viongozi wa Vyombo Vya Ulinzi na Usalama wakiwa katika hafla hiyo.
Bendi ya Polisi ikitumbuiza.
Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo.

(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni