Jumamosi, 30 Septemba 2023

MAHAKAMA YASAMBARATISHA MAWASILIANO SHIMIWI

· Tume ya Utumishi wameyataka wenyewe

Na Faustine Kapama -Mahakama, Iringa

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 30 Septemba, 2023 imeendelea kutoa dozi baada ya kuzoa pointi mbili katika kila timu kwenye mchezo wa Kamba Wanaume na Kamba Wanawake. 

Katika michezo hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Mkwawa mjini hapa, Kamba Wanaume walikutana na Mawasiliano, huku Kamba Wanawake wakikabana koo na Tume ya Utumishi na kufanikiwa kuzilambisha nyasi timu hizo.

Ulikuwa mchezo wa Kamba Wanawake ulioanza ambapo timu ya Tume ya Utumishi nusra iondolewe kwenye mashindano baada ya kuingia uwanjani kwa kusitasita wakihofia kichapo.

Mwamuzi alipouita mchezo huo, Tume ya Utumishi walijitokeza haraka haraka, lakini walipoziona ‘Tembo za Mahakama’ wakatokomea, wakidai haikuwa mechi yao.

Baada ya kujiridhisha, huku timu ya Mahakama ikiwa inasubiri mpinzani uwanjani, waamuzi waliwaita tena Tume ya Utumishi lakini wakahofia kuingia. Walipoitwa kwa mara ya tatu ndipo wakaibuka kutoka mafichoni kukabiliana na miamba ya Mahakama.

Mchezo huo ulipoanza, Mahakama hawakuwa na huruma na mtu, wakawachakaza vibaya wapinzani wao kwenye mivuto yote miwili, hivyo kuzoa pointi zote mbili.

Baadaye, mchezo wa Kamba Wanaume ulifuata kwa Mahakama kutifuana na Mawasiliano. Kipigo kikaendelea kutembea ambapo Mawasiliano walikiona cha mtema kuni baada ya kuchakazwa vibaya kwenye mivuto yote miwili.

Kufuatia ushindi huo, timu za Mahakama zinaendelea kupeperusha vyema bendera ya Mahakama, huku Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede akiwapongeza vijana wake kwa kuendeleza kile wanachokitaka.

"Kazi inaendelea, kwani bado hatujamaliza. Niwakumbushe tu wapinzani wetu kuwa vipigo kama hivi vinaendelea na yoyote tutakayekutana naye ajiandae kisaikolojia kupokea kipigo," amesema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa kuhusu mashindano haya, Mahakama Sports inatarajia kuvaana na timu zingine 14 ili kupata nafasi ya kutinga 16 bora.

Katika mpira wa miguu, timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo, timu ya netiboli ya Mahakama imepangwa katika kundi G na itapepetana na timu za Ardhi, RAS Kilimanjaro na Elimu.

Kwenye mchezo wa Kamba Wanaume, timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itaumana na TAKUKURU, RAS Kigoma, Mawasiliano na Ardhi na Kamba Wanawake imepangwa kundi A pia na itakabiliana vilivyo na timu kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri Mkuu Kazi na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Timu ya Mahakama Sports Kamba Wanawake kazi inaendelea.
Timu ya Mahakama Sports Kamba Wanaume (juu) wakiwaonyesha kazi na Mawasiliano (chini).
Timu ya Mawasiliano ikitaabika baada ya kuchakazwa vibaya. Picha chini, mchezaji wa Tume ya Utumishi akilamba nyasi baada ya kuzidiwa.

Mashabiki wa Timu ya Mahakama Sports wakishangilia baada ya wapinzani kuchezea kichapo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni