Jumamosi, 30 Septemba 2023

TIMU YA MAHAKAMA NETIBOLI MOTO, UNACHOMA

· Bendera ya Mahakama juu SHIMIWI Iringa

·Elimu yakimbiwa na mashabiki wake

Na Faustine Kapama -Mahakama, Iringa

Ukichezea moto utakuunguza. Ndicho inachokifanya Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mkoani hapa.

Katika mchezo huo uliochezwa leo tarehe 30 Septemba, 2023 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, timu ya Mahakama ilikutana na timu ngumu ya Maji ambayo imeungua vibaya baada ya kupokea kichapo cha vikapu 28 kwa 16.

Mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 5:00 asubuhi ulianza kwa timu zote mbili kukamiana huku tupia tupia vikapu ikawa bandika bandua. Kila timu inapotupia, timu nyingine nayo inatupia.

Ilikuwa timu ya Elimu iliyoanza kutupia dakika za mwanzo za mchezo, lakini Mahakama Sports ikachomoa baada ya muda mfupi. Kitendo cha Elimu kutangulia kutupia vikapu kiliwaamusha wachezaji wa Mahakama na kuanza kulisakama lango la wapinzani wao.

Tupia tupia vikapu iliendelea na hadi timu zote zinaenda mapumziko, Mahakama Sports ilikuwa mbele kwa kutumbukiza vikapu 15 kwa 11. Kipindi cha pili kiliendelea kwa Mahakama kuzidisha mashambulizi na kuzidi kuwakandamiza wapinzani wao.

Baada ya kugundua utoaji wa dozi unazidi kuendelea, mashabiki wa timu ya Elimu walizima muziki na mavuvuzela yao na kutokomea kusikojulikana na kuiacha timu yao ikiendelea kubamizwa na Mahakama Sports. Hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa, Mahakama Sports ikazoa vikapu 28 kwa 16 walizoambulia Elimu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Mahakama Sport Robert Tende amesema moto waliouwasha utaendelea kuwaunguza wote wanaojitia kimbelembele kucheza nao kwenye mashindano hayo na hawatabaki salama.

“Mjomba, huu sio moto wa kifuu, ukichomeka kidole chako utaungua, tena vibaya mno. Timu yoyote itakayoingiza timu uwanjani ikubali kuvumulia maumivu, hawatabaki salama, amini nakwambia,” alisema.

Mwalimu wa timu Paul Mathias amewashukuru vijana wake kwa kupambana na kuibuka na ushindi huo muhimu dhidi ya timu hiyo ngumu. “Nawapongeza sana vijana wangu, kwa kweli hawajaniangusha. Tulipoanzia ndipo tutakapomalizia, hakuna kupoa,” alisema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa kuhusu mashindano haya, Mahakama Sports inatarajia kuvaana na timu zingine 14 ili kupata nafasi ya kutinga 16 bora.

Katika mpira wa miguu, timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo, timu ya netiboli ya Mahakama imepangwa katika kundi G na itapepetana na timu za Ardhi, RAS Kilimanjaro na Elimu.

Kwenye mchezo wa Kamba Wanaume, timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itaumana na TAKUKURU, RAS Kigoma, Mawasiliano na Ardhi na Kamba Wanawake imepangwa kundi A pia na itakabiliana vilivyo na timu kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri Mkuu Kazi na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Mashabiki wa timu ya Mahakama Sports wakiwa mitaani mjini Iringa kushangilia vipigo vinavyoendelea kutolewa na timu yao kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
Mchezaji Philomena Haule ambaye ni mtupiaji vikapu hatari akinyanyuliwa na mashabiki baada ya mchezo huo.
Mashabiki wa Mahakama Sports wakinyanyua mtupiaji kinara wa vikapu,Tatu Mawazo baada ya kumalizika kwa mchezo.
Shangwe za mashabiki zikiendelea.
Hii hapa miamba ya Netiboli kwenye mashindano ya SHIMIWI.
Mpira huooooo unatumbukia kwenye kikapu.
Mchezaji wa timu ya Mahakama akipokea pasi safi iliyozaa kikapu.
Timu ya Elimu iliyopokea kichapo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni