Jumamosi, 30 Septemba 2023

MSIBA MWINGINE MZITO SHIMIWI IRINGA

·Mahakama Sports Mpira wa Miguu yaifumua Ras Kigoma 8:0

Na Faustine Kapama -Mahakama, Iringa

Lilikuwa suala la muda tu kwa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu kuyaanza Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa kwa kishindo kufuatia mchezo wake wa kwanza kukipiga kipute na Kilimo kuahirishwa kwa sababu ya msiba.

Leo tarehe 30 Septemba, 2023 imeingia katika Uwanja wa Samora kuvaana na timu ya Ras Kigoma na kuzabua mabao nane kwa nunge kwenye mchezo uliotawaliwa na ufundi wa kimpira uliokuwa unaonyeshwa na vijana wa Mhimili wa utoaji haki.

Mchezo huo uliochezwa majira ya alasili ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, huku Mahakama Sports ikilisakama lango la wapinzani mara kwa mara. Katika mchezo huo, mshambuliaji hatari wa Mahakama Sports Martin Mpanduzi alifanikiwa kuondoka na mpira baada ya kupachika mabao matatu.

Ilikuwa katika dakika ya 12 ambayo Mpanduzi alifungulia mlango wa magori kwa timu yake kwa kupachika bao safi kutokana na pasi murua kutoka kwa kiungo punda Selemani Magawa.

Katika dakika ya 16, Magawa alitikisa nyavu za Ras Kigoma kwa kupachika bao safi baada ya shuti kali lililomshinda mlinda mlango. Mvua ya magoli iliendelea kunyesha langoni mwa Ras Kigoma baada ya Bundi kuzengea zengea eneo hilo.

Kwenye dakika ya 22 ya mchezo, Mpanduzi tena alipachika bao lingine la tatu baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Magawa kabla ya kutikisa nyavu kwa mara nyingine katika dakika ya 31.

Magawa alipachika bao lingine katika dakika ya 35, huku Nasoro Mwampamba akihitimisha karamu ya magori katika kipindi cha kwanza baada ya kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Ras Kigoma.

Katika kipindi cha pili, timu ya Mahakama Sports ilianza kucheza pasi fupi fupi na kuzidisha mashambulizi, hivyo kuendelea kulishambulia lango la wapinzani na kufanikiwa kwa muda wote kuwachezea Ras Kigoma nusu uwanja.

Katika dakika ya 50, Abdi Sasamalo alipachika mpira kwenye nyavu na kuiandikia timu yake bao la saba kabla ya dakika mbili baadaye, Gabriel Mwita akahitimisha karamu ya magori baada ya kwenda kwenye kamba, hivyo kuiwezesha timu yake kuondoka na ushindi mnono.

Wakati wa mchezo huo, mwamuzi aliwazawadia wachezaji wawili wa Ras Kigoma kadi za njano baada ya kuwachezea rafu wachezaji wawili wa Mahakama Sports.

Wachezaji wa Mahakama Sports waliosakata kambumbu ni Fahamu Kibona, Nasoro Mwampamba, Nkuruma Katagira, Emmanuel Mwamole, Akida Mzee, Kelvin Muhagama, Frank Obadia, Gabriel Mwita, Martin Mpanduzi na Seleman Magawa.

Wengine ni Abdi Sasamalo, Mbura Minja, Iman Zumbwe, Gisbert Chentro, Rashid Hamis, Devis Munubi, Seif Shamte na Ramadhani Seif. Benchi la ufundi liliongozwa na Kocha Mkuu Spear Mbwembe na Kocha Msaidizi Said Albea.

Alikuwepo pia Timu Meneja Shaibu Kanyachole, Meneja wa Vifaa Eliya Ngule na Daktari Janeth Mapunda.

Akizungumza baada ya mchezo kumalizika, Mwalimu wa timu Spear Mbwembwe amesema wachezaji wake wamecheza vizuri, ingawa hawakufuata mfumo wa pasi fupi fupi, hasa katika kipindi cha kwanza.

Amesema baada ya kuanza kipindi cha pili, vijana wake walirudi kwenye mfumo na kuanza kuonyesha kandanda safi na kucheza mpira wa kwenye vitabu, hivyo kuwafaya timu pinzani kupoteana.

“Nadhani umejionea mwenyewe katika kipindi cha pili. Kama muda wote wangecheza hivyo, hawa jamaa (Ras Kigoma) walikuwa wanakula zaidi ya goli 10. Hata hivyo, niwapongeze vijana wangu kwa kujituma na kupata matokeo haya mazuri,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede hakuwa nyuma kumwaga sifa kwa wachezaji kwa kazi nzuri waliyokuwa wanaifanya uwanjani. Amesema kuwa ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa timu yake na anaamini kila timu itakayothubutu kukanyaga uwanjani itachezea kichapo.

“Hizi ni mvua za rasharasha, mazika bado hayajaanza. Tuna timu imara sana mwaka huu, lengo letu kila timu itakayojaribu kuja uwanjani itapata dozi ya kutosha, kuliko hata hii ambayo Ras Kigoma wameipata. Tunataka wapinzani wetu watuelewe, kwa hili hatutanii, tuna maanisha, wasije wakasema hatukuwatahadhalisha,” amesema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa kuhusu mashindano haya, timu ya Mahakama Mpira wa Miguu imepangwa kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo katika kutafuta nafasi ya kutinga 16 bora.

Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Mchezaji wa Mahakama Sports Martin Mpanduzi akikabidhiwa mpira baada ya kupachika mabao matatu kwenye mchezo huo. Picha chini Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede akimpongeza mchezaji huyo.

Wachezaji wa Mahakama Sports wakishangilia baada ya kupachika bao  kwenye lango la timu pinzani. Picha chini wachezaji wakilisakama lango la Ras Kigoma.

Kipa wa Ras Kigoma akipishana na mpira baada ya Martin Mpanduzi (wa tatu kulia)  kupachika bao. 
Kipa wa Ras Kigoma akilamba nyasi baada ya mchezaji wa Mahakama Sports Seleman Magawa kwenda kwenye nyavu. Picha chini Magawa (kulia) akifuhia na wachezaji wenzake.

Mashambulizi yakiendelea. 
Kocha Mkuu wa Mahakama Sports Spear Mbwembwe akiongea na vijana wake wakati wa mapumziko. 
Mwamuzi akimpa kadi ya njano mchezaji wa Ras Kigoma baada ya kumchezea vibaya mchezaji wa Mahakama Sports. 
Mwamuzi wa pembeni akinyoosha kibendera kuashiria kuotea kwa mchezaji.

Ulikuwa mwendo wa Aziz Key leo, si mchezo.

Vyuma hivi hapa, mtu na nusu. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni