- Yatangualia 16 bora
- Tume ya Uchaguzi waula wa chuya
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake leo tarehe 1 Octoba, 2023 imefanikiwa
kutinga kwenye hatua ya 16 bora kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa baada ya kuwatoa
kamasi Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mchezo huo ambao
umechezwa majira ya saa 12.30 asubuhi kwenye Viwanja vya Mkwawa ulianza kwa
timu zote mbili kukamiana, huku Mahakama Sports ikithihirisha umahiri wake
katika mivuto yote miwili.
Katika vipindi vyote
viwili, Mahakama Sports haikuwa na huruma na mtu, hasa baada ya Tume ya Uchaguzi
kujaribu kujitutumua, lakini walishindwa kuhimiri vishindo vya watoa haki
nchini.
Hadi waamuzi wanamaliza
mchezo huo, Tume ya uchaguzi walishatepeta, hivyo kuiwezesha Mahakama Sports
kuzoa pointi zote mbili muhimu. Kufuatia matokeo hayo, timu ya Mahakama
inakwenda moja kwa moja kwenye 16 bora.
Mahakama, ambayo ilikuwa
katika kundi A imefikia hatua hiyo baada ya kushinda mechi zake zote ilizocheza
na timu pinzani za Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri Mkuu Kazi na Tume ya
Uchaguzi (NEC).
Mahakama Sports inashiriki
katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira
wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama
Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa
kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa
kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ya pili, Mpira wa Miguu Wanaume
walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni