·Usicheze na Mahakama utaumia
·TAKUKURU ulimi nje, hawaamini kilichowakuta
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Mtoto akililia wembe mpe.
Hiki ndicho walichokifanya Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba
Wanaume kwa TAKUKURU kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na
Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani hapa.
Yalipoanza mashidano,
TAKUKURU walianza kutamba mitaani kuwa wamekuja kwa kazi moja tu, kuiondosha
Mahakama, tena katika hatua za awali, hasa kwenye mchezo wa kamba.
Siku ya kupanga makundi
wakaonyesha dhahiri nia yao na kuchagua kuwa kwenye kundi moja na
Mahakama. Wakati huo wote Mahakama ilionesha nidhamu ya hali ya juu na
kuchagua kukaa kimya.
Usiku wa deni haukawii
kukucha, hatimaye siku ikafika TAKUKURU waliyokuwa wanaisubiri kwa hamu, ni leo
tarehe 2 Octoba, 2023. Lakini kipigo walichokipata hawatasahau, kwani ukicheza
na Mahakama, ambayo ni Mhimili wa Dola, utaumia.
Ilkuwa majira ya asubuhi saa
12. 30 wanamichezo wakipofurika kwenye Viwanja vya Mkwawa kushuhudia nginja ngija
hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa pande zote
mbili.
Waamuzi walipouita mchezo
huo, TAKUKURU, kama walivyokuwa wamedhamiria, waliingia uwanjani kwa mbwembwe, wakiwa
wamejiamini huku wengine wakiwa wamevaa kininja ili kuwatisha vijana wa Professor,
jambo lililovuta hisia kubwa na kushangiliwa kwa wingi kutoka kila kona na
mashabiki.
Hata hivyo, ukimya
ulitawala pale Mahakama ilipoanza kufanya mambo yake. Katika mvuto wa kwanza,
TAKUKURU walijaribu kukaza kamba, lakini wakakutana na vyuma vikiwatazama kwa
hasira kali.
Baada ya kukata pumzi na kushindwa
kuhimili mziki mzito wa Mahakama, TAKUKURU wakakubali yaishe, hivyo wakaachia pointi
moja kwenda kwa wapinzani wao katika hatua mvuto wa kwanza.
Kibao cha mashabiki
kuwashangilia TAKUKURU kiligeuka katika kipindi cha pili baada ya Mahakama
Sports kuonyesha umahiri na ukomavu wa hali ya juu katika mashindano hayo.
TAKUKURU walijaribu kujitutumua, lakini wakakumbana na kibano kikaki na kuangukia pua, wakaamua kujisalimisha mahakamani ili kupata haki wanayostahili.
Baada ya mchezo huo,
wachezaji wa TAKUKURU, huku wakipumua juu kwa juu kama samaki aliyekosa hewa mtoni,
waliondoka kwenye Viwanja hivyo kila mmoja na njia yake na kutokomea
kusikojulikana ili kukwepa aibu waliyoipata.
Ushindi huo walioupata
Mahakama Sports unawafanya kujikita kileleni mwa kundi A na wanasubiri mchezo
mmoja utakaochezwa kesho tarehe 3 Octoba, 2023 katika viwanja hivyo dhidi ya Ardhi
ili kukamilisha hatua ya kutafuta 16 bora. Katika michezo yake miwili ya mwanzo,
Mahakama ilitoa vipigo kwa RAS Kigoma na Mawasiliano.
Baada ya mchezo
kumalizika, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema watavikata
vidomodomo vya yoyote atakayejaribu kuwatunishia misuri, hasa wale wanaovamia
mashindano bila kupata baraka za wazee.
"Hawa jamaa
(TAKUKURU) walikuwa na mdomo sana, walidhani kukaa kwetu kimya wakaona
watatufanya kama wanavyotaka. Haya ni mashindano, usivamie tu bila kwanza
kupata baraka za wazee. Kila kitu kina taratibu zake sheikh.
“Hawa jamaa walikuwa
wamejisahau sana kuwa kila mji haukosi wazee. Kipigo walichokipata nadhani sasa
hawatarudia. Niwakumbushe pia kuwa usitukane Mamba kabla ya kuvuka mto,
wasirudie tena kucheza cheza na haki za watu,” amesema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni