Jumatatu, 2 Oktoba 2023

WANANCHI MKOANI KATAVI WATAKA UTOAJI ELIMU YA SHERIA UWE ENDELEVU

 Na James Kapele – Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi

 

Wananchi mkoani Katavi wameipongeza Mahakama ya Tanzania Mkoa Katavi kwa kuisimamia ipasavyo programu ya utoeji wa elimu ya sheria kabla ya kuanza kwa mashauri kwa wananchi wanaokuwa wamehudhuria mahakamani kwa shughuli mbalimbali. 

 

Wametoa pongezi hizo hivi karibuni mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe, Gway Sumaye alipokuwa akitoa elimu hiyo katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi. 

 

Wakitoa pongezi hizo wakati wa kuhitimisha programu hiyo baadhi ya washiriki wamesema Mahakama ya Tanzania imefanya jambo kubwa la kuigwa ambalo limekuwa likiwasaidia kujifunza mambo mbalimbali ya sheria ambayo hawakuwahi kuyajua kabla na hivyo kuishukuru Mahakama kwa kuona umuhimu wa kuanzisha jambo hilo.

 

“Mhe. Hakimu binafsi naomba kuipongeza Mahakama yote kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuanzisha jambo hili ambalo kwa hakika limetusaidia sana kutuongezea uelewa katika masuala mbalimbali ya kisheria ambayo hatukuwahi kuyafahamu kabla. Naoimba Mahakama jambo hili liwe endelevu kwa kuwa litatusaidia kupunguza migogoro katika jamii yetu,” alisema Mzee Kendson Mbugi aliyeshiriki programu hiyo.

 

Mahakama Mkoa wa Katavi imejiwekea utaratibu wa utoaji wa elimu kwa wananchi wanaofika Mahakamani kwa shughuli zao mbalimbali kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria kwa kila siku kabla ya kuanza kusikilizwa kwa mashauri Mahakamani ikiwa ni moja kati ya malengo mahsusi ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa kurudisha imani ya Mahakama kwa wananchi.

 

Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi waliohudhuria programu hiyo.

Mhe .Gway Sumaye .

Mzee Kendson Mbugi Mkazi wa Kijiji cha Katsunga Mkoani Katavi akitoa neno la shukrani na pongezi kwa Mahakama. Wengine ni sehemu ya wananchi walioshiriki programu hiyo.

Sehemu ya wananchi waliohudhuria programu hiyo wakifuatilia mafunzo hayo.


Aliyesimama ni moja katika ya washiriki alipokuwa akiuliza swali wakati wa majadiliano.


(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni