Jumatatu, 2 Oktoba 2023

VIKAO VYA WATUMISHI VYALETA UFANISI WA KAZI

 Christopher Msagati- Manyara

Tathmini iliyofanyika siku za hivi karibuni imeonesha kuwa vikao vya watumishi vinavyofanyika mara kwa mara vimeongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara.

Hayo yamebainika leo tarehe 02 Oktoba, 2023 katika kikao kilichofanyika asubuhi kilichowajumuisha Watumishi wa Mahakama Kuu Manyara, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mahakama ya Wilaya ya Babati pamoja na Mahakama ya Mwanzo Babati.

Aidha, kumekuwa na utaratibu wa kufanya vikao vya watumishi wa Mahakama hizo kila Jumatatu kabla ya kuanza kwa majukumu ya kila siku. Katika vikao hivi, watumishi wa Mahakama hukumbushwa na kusisitizwa mambo ya msingi katika majukumu yao ya kila siku yakiwemo masuala ya uwajibikaji, uadilifu pamoja na utoaji huduma nzuri kwa wateja ili kupunguza malalamiko yanayoepukika. 

Vikao hivi hutumika kutoa taarifa za wiki iliyotangulia yanayohusu masuala ya mashauri, rasilimali watu pamoja na utawala lakini pia kuonesha dira ya mpango kazi wa wiki inayofuata. 

Akizungumza katika kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza  amesema  “kwa sasa mambo yanaendelea kubadilika na kuwa mazuri tofauti na hapo awali, hata utoaji huduma zetu tunapata mrejesho mzuri kutoka kwa wateja na watu wa taasisi nyingine. Wateja wanahudumiwa kwa wakati, wanasemeshwa kwa lugha nzuri na hata nakala za hukumu zinatoka kwa wakati. Haya yote ni matunda ya hivi vikao tunavyofanya kila Jumatatu asubuhi,”.

Kupitia vikao hivi imebainika kuwa ufanisi wa kazi umekuwa bora zaidi miongoni mwa watumishi na kwa sababu pia ni mahali ambapo watumishi hupata nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili mbele ya viongozi wa Mahakama na uongozi huo huwapatia suluhushi au majibu ya changamoto hizo. 

Pamoja na hayo, katika vikao hivi watumishi hujifunza mambo mbalimbali yanayohusu shughuli za kila siku mahakamani na hata mambo mbali ya kijamii na kiuchumi kwa sababu watumishi wengine wenye kufahamu mambo kama hayo hutumia vikao hivi kuwafundisha wengine juu ya masuala hayo.

             

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza akiongoza kikao cha watumishi wa Mahakama Kuu Manyara. Wa tatu ni Jaji wa Mahakama Kuu Manyara, Mhe. Gladys Barthy ambaye na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo(wa kwanza kutoka kushoto).

  Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara wakifuatilia taarifa zinazotolewa katika kikao hicho.

  Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Bw.William Makori akitoa taarifa ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara katika kikao hicho.


(Habari hii imehaririwa  na Magreth Kinabo- Mahakama)

 

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni