Alhamisi, 5 Oktoba 2023

 BALOZI SANGA AWASIHI MAJAJI KUWA NA UTHUBUTU NA UZALENDO

 

Na Mwandishi wetu  IJA

 

Mwanadiplomasia mahiri na mashuhuri nchini, Mhe.Balozi Charles Sanga amewasihi Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania  na  Mahakama Kuu ya Tanzania kuzingatia uthubutu na kutokata tamaa watakapokutana na changamoto zitakazokwaza  wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

 

Balozi Sanga ametoa wito huo alipokuwa anawasilisha mada katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakati wa mafunzo Elekezi kwa  kwa Majaji wapya wanne wa Mahakama ya Rufani na 20 wa Mahakama Kuu.

 

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha IJA, yamefunguliwa Oktoba 2, 2023 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Aidha mafunzo hayo kwa upande wa Majaji wa Mahakama ya Rufani yatachukua wiki moja na kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania yatachukua wiki tatu.

 

Katika mada yake yenye anuani isemayo, "Protocol and Etiquette," kwa maana ya Itifaki na Ustaarabu, Balozi Sanga amewaambia Majaji hao kuwa uthubutu utawawezesha kufanya mambo ambayo wengine yamewashinda.

 

"Woga ni adui wa ujasiri na uthubutu, usifanye kazi kwa woga wala usiwe mwoga kutimiza wajibu wako, ujasiri utakuwezesha kutokata tamaa katika mazingira magumu, Uthubutu utakuwezesha kufanya mambo ambayo wengine yamewashinda," amesema Balozi Sanga.

 

Pia Balozi Sanga ambaye ni mmoja wa wasaidizi wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, amewashauri Majaji hao kuwa wazalendo kwa nchi yao na kutenda kazi zao kwa uweledi, haki na uadilifu.

 

"Utaifa na uzalendo ni kuwa na moyo uliotukuka kwa nchi na wananchi wake, hivyo jipambeni na sifa hizo ambazo zitawafanya mtekeleze majukumu yenu kwa uweledi na uadilifu huku pia mkizingatia maslahi ya taifa lenu," ameongeza Balozi Sanga.

 

Kuhusiana na masuala ya itifaki, Balozi Sanga amewapitisha Majaji hao kwenye kanuni mbalimbali zinazohusu taaaluma hiyo ili wazitambue na  hivyo kutopata ugumu pale wanapokutana na masuala yahusuyo itifaki na ustaarabu.

 

Majaji hao wapya waliteuliwa na Rais  wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo tarehe 03 Septemba, 2023 na kuapishwa tarehe 14 Septemba,2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.

 



Balozi Charles Sanga akiwasilisha mada katika mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na  wa Mahakama Kuu ya Tanzania yanayofayika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wilayani Lushoto mkoani Tanga.


   (Habari hii imehaririwa  na  Magreth Kinabo- Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni