Alhamisi, 5 Oktoba 2023

JAJI KIHWELO: MAJAJI MTEGEMEENI MUNGU KATIKA KAZI ZENU

 Na Mwandishi wetu IJA

 

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul  Kihwelo amewanasihi Majaji wapya wa Mahakama kuu ya Tanzania kumtegemea  Mwenyezi Mungu, kwa kuwa kazi zao ni nzito, na hivyo zinahitaji msaada mkubwa wa Mungu ili kuweza kuzitekeleza kwa uadilifu na haki. 

 

Mhe. Kihwelo amesema hayo Oktoba 03, 2023, alipokuwa anawasilisha mada katika mafunzo elekezi kwa Majaji hao, ambayo yanafanyika katika Chuo cha IJA wilayani Lushoto mkoani Tanga.

 

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha IJA, yalifunguliwa Oktoba 02, 2023 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

 

Katika nasaha zake, Mhe. Jaji Kihwelo amesema: "Mimi huwa nasema hii kazi ya Ujaji ni kazi ya Mwenyezi Mungu, hivyo tumtegemee  yeye, huu utakuwa ni muongozo kwetu kutoa uamuzi wenye busara pale tunapotoa hukumu zetu. Ukimtegemea  Mwenyezi Mungu ni sawa na kinga yako pia, tumuombe mwenyezi Mungu s kila mtu kwa imani yake,"amesema.

 

Kwa upande mwingine, Mhe. Kihwelo amewahimiza Majaji hao kuwa wanyenyekevu na kuishi na watu vizuri wakiwemo wasaidizi wao wa kazi za Mahakamani na kwengineko.

 

"Ishi na watu vizuri na Be humble (kuwa mnyenyekevu), hii mimi binafsi imenisaidia, pia tusijiweke mbali  na wasaidizi wetu, wao ndio wanatusaidia katika kazi zetu," amehimiza Mhe. Jaji Kihwelo.

 

Mhe. Jaji Kihwelo amewasilisha mada yenye anuani isemayo, "Judicial Culture: What is it and how does it differ with other cultures," kwa tafsiri isiyo rasmi  "Utamaduni wa Mahakama: Ni kitu gani na unatofautiana vipi na tamaduni zingine,"  ambapo amewaambia Majaji hao kuzingatia utamaduni wa Mahakama ya Tanzania ili iwasaidie kufanya kazi zao kwa ufanisi na bila shida.

 

Majaji hao wapya waliteuliwa na Rais  wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo tarehe 03 Septemba, 2023 na kuapishwa tarehe 14 Setemba,2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul  Kihwelo  akitoa mada.


Majaji wakiwa katika mafunzo hayo.



(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni