·Yanyayua makwapa mshindi wa pili Riadha, Tufe
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) imeanza kunyayua makwapa katika Mashindano ya
Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea
mkoani hapa baada ya kufanya vizuri kwenye michezo ya riadha wanawake na tufe
wanaume.
Katika mchezo wa riadha,
Mahakama Sports imeshika nafasi ya pili kwenye mita 3,000 baada ya mfukuza wake
upepo Justa George, maarufu kama MMM kuwatimulia vumbi wapinzani wake. Justa
pia aliipeleka Mahakama fainali kwenye mita 100.
Kadhalika, mfukuza upepo
mwingine maarufu wa Mahakama Sports Upendo Gustaf aliipeperusha vyema bendera
ya Mahakama kwenye mita 200 na 400 na kufanikiwa kutinga fainali baada ya
kushika nafasi ya pili kwenye michezo hiyo.
Kwa upande wa wanaume,
Martin Mpanduzi alipepetana na wapinzani wake kwenye mita 100 na kufanikiwa
kutinga nusu fainali baada ya kukamata nafasi ya pili. Hata hivyo, aliondoshwa
kwenye kinyang’anyiro wakati wa kwenda fainali baada ya kuteleza wakati anaanza
kutimua mbio.
Katika upande wa mchezo
wa tufe, Martin Mushi alifanya vizuri na kushika nafasi ya pili baada ya kuzoa
pointi 9.05, akimfuatia mpinzani wake wa karibu aliyepata pointi 9.44. Kufuatia
ushindi huo mnono, Mahakama Sports imejihakikishia hadi sasa kuweka kibindoni
medali mbili.
Akizungumza kufuatia
matokeo hayo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza vijana
wake kwa kupeperusha vyema bendera ya Mahakama ya Tanzania kwenye michezo hiyo.
Amesema hatua
waliyofikia ni nzuri na wanatarajia kufanya vizuri pia kwenye michezo mingine. "Kama
nilivyosema awali, huu ni mwanzo mzuri na tutaendelea kukusanya makombe na
medali kwenye michezo mingine. Hatua tuliyofikia kwa sasa ni nzuri,
"amesema.
Mahakama Sports imepeleka timu nne kwenye hatua ya 16 bora baada ya kufanya vizuri kwenye makundi. Michezo hiyo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Netiboli na Mpira wa Miguu Wanaume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni