Alhamisi, 5 Oktoba 2023

MAHAKAMA YA TANZANIA KUWA MWENYEJI MKUTANO MKUU WA 'SEACJF'

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa  Afrika (SEACJF) utakaofanyika tarehe 23 Oktoba, 2023. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika hadi tarehe 27, Oktoba mwaka huu katika Hoteli ya 'Mount' jijini Arusha.

Akizungumza hivi karibuni na Wahariri na Waandishi kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari nchini, Mwenyekiti wa Kamati ya  Maandalizi ya Mkutano huo ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ignas Kitusi alisema  Mkutano huo utahudhuriwa na Majaji Wakuu 16 kutoka Angola, Botswana, Eswatin, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania Bara, Tanzania Visiwani (Zanzibar), Uganda, Zambia na Zimbamwe.

“Jukwaa hili pia ni sehemu ya kujadiliana juu ya changamoto zinazowakabili katika mfumo wa utoaji haki na kubadilishana mbinu bora na kushughulikia changamoto zinazokabili Mahakama katika Nchi zetu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mhe. Kitusi Kaulimbiu ya Mkutano huo ni “Wajibu wa Mahakama za Kitaifa katika Utatuzi wa Migogoro kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA): Matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni