·Yatoshana nguvu na Kilimo
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu leo tarehe 4 Octoba, 2023 imetoshana
nguvu kwa kutoka suluhu na timu ya Kilimo katika mchezo ambao ndiyo ulikuwa wa ufunguzi
rasmi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayoendelea mkoani hapa.
Mchezo huo uliochezwa
majira ya mchana katika Uwanja wa Samora ulikuwa ni wa upinzani mkali, huku
timu zote zikishambuliana zamu kwa zamu. Katika mchezo huo, Mahakama Sports
ilicheza kandanda safi kwa pasi fupi fupi, lakini wapinzani wao walikuwa imara
katika kuzuia mashambulizi.
Hadi kipindi cha kwanza
kinamalizika, hakuna timu iliyokuwa imeliona lango la mwenzie. Katika kipindi
cha pili timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, lakini kabumbu lilichezwa
zaidi katikati, hivyo kuzuia hatari yoyote kwenda kwenye lango la timu pinzani.
Katika kipindi hicho cha
pili, mchezaji mmoja wa Kilimo alizawadiwa kadi ya njano kwa kumchezea mchezaji
wa Mahakama Sports rafu. Hadi mwamuzi anamaliza mtanange huo, timu zote mbili
zilitoka uwanjani bila kufungana.
Kwa matokeo hayo, Mahakama
Sports inakwea kileleni mwa kundi A na kushika nafasi ya kwanza kwa kushinda
mechi mbili, kutoka sale mchezo mmoja na kupewa ushindi mchezo mmoja baada ya timu ya Maji kuchezesha mamluki.
Wachezaji walioiwakilisha
Mahakama ni Micheal Turuka, Nasoro Mwampamba, Akida Mzee, Kelvin Muhagama,
Frank Obadia, Gabriel Mwita, Martin Mpanduzi na Seleman Magawa, Abdi Sasamalo,
Mbura Minja, Iman Zumbwe, Rashid Hamis, Devis Munubi na Gisbert Chentro.
Wengine walikuwa Seif
Shamte, Nkuruma Katagira, Emmanuel Mwamole Fahamu Kibona na Ramadhani Seif.
Benchi la ufundi liliongozwa na Kocha Mkuu Spear Mbwembe na Kocha Msaidizi Said
Albea, Timu Meneja Shaibu Kanyachole, Meneja wa Vifaa Eliya Ngule na Daktari
Janeth Mapunda.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko akimkabidhi mpira Nahodha Msaidizi wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Seleman Magawa (kulia) kama ishara ya uzinduzi rasmi wa Mashindano ya SHIMIWI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni