Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe.Dkt. Dotto Biteko leo tarehe 4 Octoba, 2023 amefungua rasmi Mashindano
ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika
mkoani hapa na kuwahimiza Viongozi katika Wizara, Taasisi, Wakala zinazojitegemea na Mamlaka
za Serikali za Mitaa kushiriki kimamilifu kwenye mashindano
hayo wao wenyewe.
Akizungumza katika Uwanja
wa Samora kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan baada ya kupokea maandamano ya wanamichezo kutoka Taasisi
mbalimbali wanaoshiriki kwenye mashindano hayo, Waziri Biteko alieleza kuwa
Viongozi wote wasichukulie
mashindano hayo kama jambo dogo.
“Tusichukulia hili kama jambo dogo na wanaotakiwa
kushiriki ni watu wa aina fulani na kwamba sisi tunayo makubwa zaidi kuliko
haya. Ni imani yangu mwaka unaokuja sisi Viongozi tushiriki kikamilifu, hata
kama tuna dharura, basi tupange vizuri ratiba zetu ili watumishi hawa waweze
kufurahi kuwaona Viongozi wao wanashirikiana pamoja katika kuendeleza michezo,”
amesema.
Amewakumbusha Viongozi wa Serikali kuwa watumishi
wa umma ndiyo nyenzo kubwa ya maendeleo nchini Tanzania, hivyo inapotokea fursa
ya kushiriki na wengine kwenye michezo ni muhimu kuwawezesha kikamilifu na kwa
Viongozi kushiriki wao wenyewe, hatua itakayowafanya watambue kuwa michezo
inathaminiwa.
“Tuwawezeshe kikamilifu wale wote ambao wanastahili
kuja kwenye michezo. Haina maana yoyote watu hawa wametoka katika Mikoa mbalimbali
kuja kushiriki katika michezo, halafu waishi kwa taabu kama watu waliopewa
lift, hapana. Fedha mnazozitenga siyo hasara, bali zitakuwa faida na faida
yenyewe mtaiona wakirudi kwenye ofisi zao,” amesema.
Kadhalika, Mhe, Dkt. Biteko amezihimiza Wizara, Mikoa,
Taasisi na Idara na Wakala za Serikali kutokurudi nyuma katika kuwapa ruhusa
watumishi wa umma ambao wapo tayari kushiriki katika mashindano hayo, hivyo
wanapaswa kujitathmini ili kutambua umuhimu wa michezo hiyo kwa ajili ya
maslahi makubwa na kuongeza tija mahala pa kazi.
Amerejea malengo ya mashindamo hayo ambayo,
pamoja na mambo mengine, yanalenga siyo tu kuboresha afya na akili, bali pia kuboresha
mahusiano mazuri ya kikazi pamoja na mtandao wa kiutumishi miongoni mwa
washiriki wote. Hivyo, ameupongeza uongozi wa SHIMIWI na wanamichezo wote kwa
kuhakikisha kuwa michezo hiyo inaendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka.
Awali, akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu
kuzungumza na wanamichezo wote, Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Mwalusamba alieleza
kuwa kwa mwaka huu wa 2023, mashindano hayo yanajumuisha jumla ya washiriki 2765
kutoka kwenye Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali na kati ya hao wanaume ni
1570 na wanawake ni 1135 ambao wanaoshiriki katika michezo mbalimbali.
Alieleza kuwa wanamichezo hao wameanza kushiriki
katika michezo mbalimbali kuanzia tarehe 29 Septemba, 2023 na michezo hiyo
inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 14 Octoba, 2023. Mwenyekiti ametaja michezo ambayo
watumishi wanashiriki ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Mpira wa Miguu,
Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha pamoja na vinyoya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Rehema Tendegu amewakaribisha wanamichezo wote mkoani kwake na kuwahakikishia usalama wakati wote. Kadhalika, amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa ukarimu wanaouonesha kwa wanamichezo hao na kuwaomba kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni