·Zatinga robo fainali kibabe
·Tume ya Uchaguzi, Mifugo wasurubishwa, wafungasha virago
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu za Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume na Kamba Wanawake zimefanikiwa kuingia
robo fainali kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI)yanayofanyika mkoani hapa baada ya kuzisurubisha timu za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mifugo.
Michezo yote mawili katika
hatua ya mtoano ya 16 bora imechezwa leo tarahe 6 Octoba, 2023 katika viwanja
vya Mkwawa. Ulikuwa mchezo wa Kamba Wanawake ulioanza ambapo Mifugo walionekana
kujiamini, hasa baada ya mashabiki kuwashangilia wakati wanaingia
uwanjani.
Hata hivyo, kibao
kiliwageukia Mifugo wakati mchezo ulipoanza baada ya Mahakama Sports kuwasurubu na kupokea kichapo katika mvuto wa
kwanza. Utoaji wa vichapo uliendelea pia katika hatua ya pili ambapo Mahakama
Sports haikuwa na huruma na mtu na kufanikiwa kuwaondoa Mifugo kwenye
mashindano baada ya kuzoa pointi zote mbili.
Baada ya mchezo huo
kukamilika ilifuata Kamba Wanaume ambapo Mahakama Sports ilipangwa kuchakachuana
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume waliingia kwenye mchezo wakiwa hawana amani,
hasa baada ya kuiona miamba ya Mahakama ikiwa imesimama imara.
Katika mivuto yote
miwili, Mahakama Sports iliwasambaratisha Tume na kujikuta wanalambishwa nyasi
baada ya kujaribu kuleta upinzani kwa magwiji hao wa mchezo wa kamba nchini.
Kufuatia matokeo, timu
zote mbili za Mahakama Sports Kamba Wanaume na Kamba Wanawake zinatangulia robo
fainali, hivyo kuzifanya timu pinzani Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mifugo kuyaaga
mashindano.
Akizungumza baada ya
michezo hiyo miwili, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema kazi
ndiyo imeanza. Amesema kila timu watakayokutana nayo katika hatua ya mtoano
itapokea kichapo kikali.
"Sisi ni watoa haki,
hivyo hatupendelei mtu yoyote, hivyo kwetu sisi vichapo ni vya kila mtu. Kuna
watu walikuja na vidomodomo, tayari tumeshavikata. Kwa hiyo, yoyote atakayekuja
ajiandae kabisa kuchezea kichapo, tutambamiza mtu yoyote atakayejipendekeza,"
amesema.
Mahakama Sports imepeleka
timu nne kwenye hatua ya 16 bora baada ya kufanya vizuri kwenye makundi.
Michezo hiyo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Netiboli na Mpira wa Miguu
Wanaume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni