Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Bukoba
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher
Siyani amewataka wananchi na wadau wengine wa utoaji haki kutoingilia au
kuvamia maeneo ya Mahakama kwa kuwa kitendo cha kujitwalia maeneo hayo kinaathiri
mipango ya Mahakama ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
Akizungumza leo mjini Bukoba wakati wa Mkutano wa Tume na
wadau wa utoaji haki, Jaji Kiongozi alisema kuwa jumla ya Mahakama za Mwanzo 29
nchini zinakabiliwa na migogoro kwa wananchi kuvamia maeneo hayo lakini
Serikali za maeneo husika huamua kuyagawa kwa sababu mbalimbali.
Jaji Kiongozi ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona wananchi, Serikali
za Vijiji na Kata wanatambua maeneo ya
Mahakama na kuyalinda.
’Nchi yetu ina Tarafa 560 na Kata 3,956, lengo la Mahakama
ni kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa na Mahakama za Mwanzo kwenye kila
Tarafa na baadaye kila Kata. Hadi sasa tunazo Mahakama za Mwanzo 946 na kati ya
hizo 167 hazifanyi kazi kwa sababu mbalimbali na 212 zinatembelewa”, alifafanua.
Alisema kuwa wananchi takribani 3,010 wanalazimika
kufuata huduma za haki kwenye Kata nyingine, hivyo Mahakama na Serikali
inafanya juhudi ili malengo ya kuwa na Mahakama kwenye kila Kata yatimie. Alisema
kwa mwaka huu, jumla ya majengo 60 ya Mahakama za Mwanzo 60 yanatarajiwa kujengwa
nchini kote.
Aidha, Jaji Kiongozi pia amezitaka Taasisi wadau wa
Mahakama zinazofanya tafiti kuhusu Mahakama na huduma inazozitoa kuzingatia weledi
katika ufanyaji wa tafiti hizo na kuihusisha Mahakama pale inapobidi ili
matokeo ya tafiti hizo yawe sahihi na yenye athari chanya zitakazosaidia ujenzi
wa taasisi imara inayotoa huduma bora.
”Matokeo ya utafiti yasiyo sahihi au taarifa zinazotolewa
za wadau bila utafiti zinaweza kuwa na athari hasi kwa taasisi kama Mahakama,
ambayo mtaji wake mkubwa ni imani ya wananchi inaowahudumia”, alisema.
Kuhusu uwepo wa Mawakili Vishoka, Jaji Siyani amewataka wadau
wote wanaotumia huduma za mawakili kuhakiki Mawakili kwa kutumia mfumo wa
e-Wakili kabla ya kuwaajiri. Alisema Mwananchi anaweza kutumia simu janja kwa
kuandika jina la wakili au namba yake ya
usajili ili kujiridhisha juu ya uhalali wake.
Aliwataka Mawakili wote nchini kujenga utamaduni wa
kutambuana kabla ya kuingia mahakamani kwa kutumia mfumo huo ambao umejengwa na
Mahakama kwa manufaa ya wote. Alisema kuwa mfumo huo ukitumika vizuri utaondoa tatizo
la watu wasio na sifa za uwakili maarufu kama vishoka kuendelea kuwahujumu
wananchi kwa kuwadanganya kuwa ni Mawakili wakati sio.
Wadau wa Utoaji Haki mkoani Kagera wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo mkoani Kagera.
Wadau wa Utoaji Haki mkoani Kagera wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo mkoani Kagera. Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Utoaji Haki mkoani Kagera. Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika, akifuatiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani. Wa pili kulia ni Mhe. Bahame Tom Nyanduga na kulia ni Mhe. Dosca Mutabuzi.
Naibu Makatibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Utoaji Haki mkoani Kagera. Kushoto ni Bi. Enziel Mtei (Ajira) na kulia ni Bi. Alesia Mbuya (Nidhamu na Maadili).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni