Jumanne, 10 Oktoba 2023

MAHAKAMA SPORTS YATAMBA MCHEZO WA BAO SHIMIWI

·Yabeba kombe mshindi wa pili wanaume

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa 

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mchezo wa Bao leo tarehe 10 Octoba, 2023 imepeperusha vyema bendera ya Mahakama ya Tanzania kwenye mchezo wa bao baada ya kushika nafasi ya pili kwa upande wa wanaume.

Mchezo huo uliochezwa katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Kikristo Ruaha kuanzia saa 2:00 asubuhi umemuinua kijana machachari, Hashim Rashid na kushika nafasi hiyo baada ya kuwabwaga wapinzani wake kutoka katika hatua ya makundi hadi fainali.

Kutokana na matokeo hayo, Mahakama Sports inanyakua kombe la kwanza kwenye mashindano hayo, huku tayari imeshaweka kibindoni medali tatu, mbili katika mchezo wa riadha na moja kwenye kurusha tufe.

Wanawake pia walishiriki katika mchezo huo kupitia Filomemna Haule ambaye alifanya vizuri kuanzia kwenye makundi na kufanikiwa kuwakimbiza mchaka mchaka wapinzani hadi hatua ya robo fainali alipoteleza.

Kitu cha kushangaza katika mchezo huo, mshindi wa kwanza ambaye ni Ras Lindi alipata vipigo mara mbili kutoka kwa Philomena, ambaye hakuwa na uzoefu wowote kwenye mchezo huo kwani ni mara yake ya kwanza kushiriki.

Kwa upande wa wanaume, Rashid alianza mashindano kwenye mchezo huo kuanzia makundi kwa kukabana koo na Madini ambao walitokashana nguvu sawa na baadaye akakutana na Uchukuzi ambaye alimgalagaza vibaya.

Kwenye mchezo wa mwisho hatua ya makundi, Mahakama Sports ilikutana na Ras Kigoma ambapo Rashid alimshikisha adabu mpinzani wake na kutinga katika hatua ya 16 bora.

Katika hatua hiyo, Mahakama Sports ilikutana na mwajiri wake, Tume ya Utumishi wa Mahakama. Mpambano kati ya Baba na Mwana ulikuwa mkali, lakini mwisho Baba akakubali yaishe na kufungashiwa vilago na Mwana kwenye mashindano. 

Matokeo hayo yaliipeleka Mahakama Sports robo fainali na kukutana na Ras Ruvuma, ambaye walikutana kwenye mashindano ya Mei Mosi Morogoro katika hatua ya fainali na kuibuka mshindi.

Katika mchuano wa leo, Ras Ruvuma ameangukia pua na kutupwa nje ya mashindano, hivyo kuiwezesha Mahakama Sports kutinga nusu fainali. Kwenye hatua hiyo, Mahakama Sports imechuana na Kilimo ambao nao wakachemsha.

Baada ya kuingia hatua ya fainali, Mahakama Sports ikacheza na Ujenzi ambao walikiona cha moto baada ya Rashid kutembeza makoleo hapa na pale, ingawa bahati haikuwa yake na kuishia kushika nafasi ya pili.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza wachezaji wake kwa mchezo na ushindani mzuri waliouonesha kwa kipindi chote.

“Haya ni mafanikio makubwa sana kwetu. Nampongeza sana Philomena, hii ni mara yeke ya kwanza kushiriki na hakuwa na uzoefu wowote kwenye mashindano haya, lakini mmeona alichokifanya. Ninaamini mwakani atafanya maajabu.

“Vile vile nampongeza sana mchezaji wetu Hashimu, hatua aliyofikia mwaka huu ni kubwa sana ukilinganisha na mwaka jana ambapo alishika nafasi ya kwanza. Kwa mwendo huu mwakani tutashika nafasi ya kwanza. Hivyo, nawapongeza wote kwa kuiheshimisha Mahakama ya Tanzania,” amesema.

Kesho tarehe 11 Octoba, 2023, Mahakama Sports inajitupa kwenye michezo minne kwenye hatua ya nusu fainali. Michezo hiyo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Netiboli na Mpira wa Miguu Wanaume.

Mwamba huyu hapa, Hashim Rashid. Mtaalam wa mchezo wa bao.

Mwingine huyu hapa, Philomena Haule. Naye mambo safi.

Hashim Rashid (kushoto) akimchachafya jamaa wa Uchukuzi, picha chini Philomena (kulia) akimwendesha puta mchezaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni