Jumatano, 11 Oktoba 2023

KASI YA UMALIZWAJI WA MASHAURI YAWAKOSHA WADAU WA HAKI JINAI SINGIDA

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Wadau wa Haki Jinai mkoani Singida wamempongeza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Juliana Masabo kwa kasi ya umalizwaji wa mashauri ya Mahakama Kuu yaliyokuwa yakiendelea kusikilizwa mkoani humo kuanzia tarehe 25 Septemba, 2023 hadi tarehe 10 Oktoba 2023. 

Pongezi hizo zimetolewa katika kikao cha kuhitimisha usikilizaji maalum wa mashauri ya jinai mkoani humo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida. 

Akisoma taarifa fupi katika kikao hicho, Msaidizi wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Getrude Misana alisema, “kikao maalum cha kusikiliza Mashauri ya jinai mkoani Singida kilianza rasmi tarehe 25 Septemba 2023 na kilikadiriwa kuhitimishwa tarehe 23 Oktoba 2023 kikiwa na idadi ya mashauri 13 lakini kutokana na ushirikiano kutoka kwa wadau kikao kimehitimishwa tarehe 10 Oktoba 2023 na mashauri 11 yamemalizwa, mashauri mawili (2) yameshasikilizwa na kupangwa kutolewa hukumu tarehe 30 Novemba, 2023”. 

Naye, Mhe. Masabo amewashukuru wadau kwa ushirikiano waliouonesha na kuhakikisha kuwa, muda unatumika vizuri ili haki iweze kutolewa kwa wakati kwani ndio jukumu kubwa la Mahakama. Aidha, amewataka radhi wadau hao pale alipokwenda kasi zaidi kinyume na matarajio yao kwani ilikuwa ni sehemu ya kuhakikisha muda unatumika ipasavyo pasipo kuupoteza.

Akihitimisha kikao hicho, Jaji Mfawidhi amewataka wadau kujipanga zaidi kwani Mkoa wa Singida unatarajiwa kuwa na vikao maalum vingine viwili katika miezi ya Novemba na Desemba mwaka huu na ratiba ya mashauri ‘cause list’ imeshatolewa.

“Sambamba na hili, Mkoa wa Singida unategemewa kuwa na vikao vingine viwili kwa mwezi Novemba na Desemba mwaka huu hivyo ,tujiandae,” alisema. 

Wadau wa Haki jinai mkoani Singida wakiwa katika kikao cha kuhitimisha vikao maalum vya Mahakama Kuu vilivyofanyika mkoani humo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyesimama mbele) akizungumza na Wadau (hawapo katika picha) katika kikao cha kuhitimisha vikao maalum vya Mahakama vilivyofanyika mkoani Singida. Kushoto kwa Jaji Mfawidhi ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa.

Wakili wa Serikali, Bi. Caren Rwebangula (aliyesimama) akitoa pongezi mbele ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (hayupo katika picha).

Wakili wa Serikali, Bw. Hussein (aliyesimama) akitoa salamu za pongezi kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (hayupo katika picha).

Wakili wa kujitegemea, Bw. Jackson Mayeka aliyesimama akitoa salamu za pongezi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma,  Mhe. Dkt. Juliana Masabo (hayupo katika picha).

Wakili wa Kujitegemea, Bw. Salma Mussa (aliyesimama) akitoa salamu za pongezi kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (hayupo katika picha).

Mtendaji  Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Mhoja Kasuka (aliyesimama nyuma mwenye kizibao cheupe) akitoa salamu za pongezi kwa Jaji Mfawidhi,  Mhe. Dkt. Juliana Masabo (hayupo katika picha).

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni