·Viwanda wanaume naye aburutwa
·Ras Kagera wanawake ulimi nje
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu za Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume na Kamba Wanawake zimetangulia fainali
kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa.
Mahakama Sports Kamba
Wanaume wamewabamiza Viwanda, huku Wanawake wakitoa kipigo kikali kwa Ras
Kagera. Michezo yote miwili imechezwa saa 12:30 asubuhi katika viwanja vya
Mkwawa.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia
Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Stephen Magoha ameshuhudia michezo hiyo na kupongeza
vijana wake kwa ushindi mnono walioupata. Amewatia moyo kuendelea kupambana ili
kunyakua makombe yote.
Ulikuwa mchezo wa Kamba Wanawake
ulioanza kuchezwa huku Ras Kagera wakijaribu kuonyesha upinzani katika sekunde
za mwanzo na kujipa matumaini kuwa wangeweza kushinda mchezo huo.
Kumbe ilikuwa danganya
toto bwana, kwani Mahakama Sports walikuja juu na kuwasambaratisha vibaya wapinzani
hao katika mvuto wa kwanza, hivyo kujihakikishia pointi moja.
Katika mvuto wa pili, Ras
Kagera walionekana kutepeta na baada ya kushushiwa kipigo kikali walipoteana na
kupoteza mpambano huo. Hadi mwisho wa mchezo ambao haukuchukua muda mrefu,
Mahakama Sports ikaondoka na pointi zote mbili.
Baada ya mchezo huo
kukamilika, ilifuata Kamba Wanaume ambapo Mahakama Sports iliwapigisha chafya
Viwanda baada ya kuwapelekea pumzi ya moto na kutoa kichapo cha mwizi wa bata,
hivyo kupoteza mchezo katika mivuto yote miwili.
Katika mchezo huo, Viwanda
waliingia uwanjani wakiwa wamejiamini kwa nia ya kuwaaibisha Mahakama Sports.
Hata hivyo, baada ya mchezo kuanza walikumbana na upinzani mkali na kuburutwa
walipojaribu kujitutumua.
Kufuatia matokeao hayo,
Mahakama Sports Kamba Wanaume watakutana na pacha wake, watoto wa Baba mmoja,
Ikulu ambao wametinga katika hatua hiyo baada ya kuwang’oa Uchukuzi, huku
Wanawake wakikutana na Uchukuzi ambao wamewashinda Ras Iringa kwa taaabu.
Katika michezo ya leo, Kamba
Wanaume iliundwa na Leonard Kazimzuri, Joseph Chokela, Cletus Yuda, Luyuga
Luyuga, Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Abdulmumin Mbaraka, John Charles, Kumbukeni
Mtete na Martin Mushi.
‘Super Sub’ walikuwa Hemed
Semith, Emmanuel Dasian, Ashel Chaula, Willy Mwaijibe, Mussa Komba na Marko
Mochiwa.
Kwa upande wa Kamba
Wanawake walikuwepo Judy Mwakyalabwe, Zahara Suleiman, Beatrice Dibogo, Melina
Mwinuka, Rebeca Mwakabuba, Tumaini Kizito, Namweta Mcharo, Joyce Simba,
Sarafina Mkumbo na Mariam Mayalla.
Waliosimama kwenye mbao
ndefu walikuwa Winiel Mahumbuga, Witness Lyasato, Veronica Rajabu, Eunice
Lugiana na Janeth Mapunda.
Timu zote zipo chini ya
Viongozi wa Mahakama Sports ambao ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti
Fidelis Choka, Katibu Robert Tende, Naibu Katibu Theodosia Mwangoka na Mweka Hazina
Rajab Ally.
Wengine ni Meneja wa Timu
Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile, Mjumbe Rajabu Mwaliko na Mjumbe
Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni