Jumatatu, 9 Oktoba 2023

JAJI MFAWIDHI AKAGUA MAHAKAMA 42 MKOANI SIMIYU KWA SIKU TANO

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali hivi karibuni alifanya ziara ya siku tano kukagua shughuli za kimahakama katika Mahakama zote 42 zilizopo Mkoa wa Simiyu.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mahimbali aliongozana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita pamoja na Katibu wake, Mhe. Dushi Lugoye.

Akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara yake, Jaji Mfawidhi alihimiza Mahakimu kufunga mashauri ya mirathi yaliamuliwa baada ya miezi minne kukamilika.

Kadhalika, Mhe. Mahimbali aliwaaziagiza Viongozi wa Mahakama katika ngazi zote kudhibiti mipaka ya viwanja vya Mahakama na kurejesha maeneo yaliyonyang’anywa.

Alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji na kuendeleza ushirikiano baina yao, kutumia rasilimali kwa uangalifu na ubunifu ili kufikia adhma ya Mahakama ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Niwapongeze wote kwa kujituma na kazi kubwa mnayoifanya, kwani licha ya kuwa na mazingira magumu ya kazi na kwa uchache wenu bado mnafanya kazi ya kuhakikisha mnatoa huduma bora,” aliwaambia watumishi wa Mahakama.

Akiwa katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi alihimiza utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu la kuongeza kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuhakikisha kila Mahakama ya Mwanzo inawekewa huduma ya umeme.

Mhe. Mahimbali pia alisisitiza matumizi ya watumishi wa kada moja kufanya kazi za kada nyingine ili kujengea uwezo mwingine wa watumishi hao.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu aliwasilisha shukrani kwa niaba ya Mkoa wa Simiyu kwa ujio wa Jaji Mfawidhi na aliahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali alioongozana nao katika ziara yake, akiwemo Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu Mhe. Martha Mahumbuga (kushoto).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (katikati aliyeshika diari nyekundu) akikagua maeneo ya Mahakama Wilaya ya Maswa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akisikiliza taarifa ya kituo cha Mahakama ya Mwanzo Itinje Wilaya ya Meatu.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Maswa (aliyesimama) akimsomea taarifa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (aliyekaa mbele) na pembeni ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akithitimishi ziara yake katika viwanja vya Maswa.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni