·Yafanyiwa figisufigisu mbio za kupokezana vijiti
Na Faustine
Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) imenyakua medali nyingine kwenye Mashindano ya
Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea
mkoani hapa baada ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa riadha wanawake.
Katika mchezo huo
uliochezwa majira ya saa 12:30 asubuhi leo tarehe 9 Octoba,2023, Mahakama
Sports imeshika nafasi ya pili kwenye mita 400 baada ya mkimbiaji wake hatari
Upendo Gustaf kuwatimulia vumbi wapinzani wake.
Mahakama pia ilishiriki
kwenye mbio za kupokezana vijiti wanawake na mfukuza upepo Justa George
aliyekamata kijiti kwa mara ya mwisho alifanikiwa kushika nafasi ya kwanza,
lakini akaondolewa kwenye kinyang’anyiro kwenda fainali.
Waamuzi walidai kuwa
wakati anakimbia, Justa alitoka kwenye mstari wake, jambo ambalo siyo kweli.
Hata hivyo, Viongozi wa Mahakama Sports wameamua kuivalia njuga figisufigisu hiyo
ili haki iweze kutendeka.
Kadhalika, wanaume pia walishiriki
kwenye mbio hizo kufanikiwa kuingia nuzu fainali. Waliondolewa baadaye kwenye
mashindano kuelekea fainali baada ya mchezaji wake wa kwanza kushika kijiti kuchelewa
kuchomoka kwenye mstari.
Hii ni mara ya pili kwa
Mahakama Sports kuzoa medali kwenye mashindano hayo. Medali zingine ambazo
tayari imeshaweke kibindoni ni riadha mita 3,000 wanawake kupitia kwa Justa George
aliyeshika nafasi ya pili na tufe kupitia kwa Martin Mushi ambaye naye
alinyakua nafasi ya pili.
Mahakama pia imefanikiwa
kuingia fainali kwenye mbio za mita 100, mchezo ambao unatarajiwa kuchezwa kesho
tarehe 10 Octoba, 2023.
Akizungumza kufuatia matokeo
hayo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza vijana wake kwa
kupeperusha vyema bendera ya Mahakama ya Tanzania na anaamini watafanya vizuri
kwenye mchezo uliobakia.
Amesema wataendelea
kupambana pia kwenye michezo mingine ili kuweza kufanya vizuri na kuchukua
vikombe. Mahakama Sports imeshaingiza tayari michezo minne kwenye hatua ya nusu
fainali. Michezo hiyo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Netiboli na Mpira wa
Miguu Wanaume.
Mwanamichezo wa Mahakama Sports, Upendo Gustaf (wa pili kutoka kulia) akikabana koo na mpinzani wake wakati wa kumalizia mbio za mita 400.
Upendo Gustaf akiongozwa na mwamuzi baada ya kumaliza mbio za mita 400. Picha chini akiandikisha jina kwa waamuzi wengine.
Justa George ( wa kwanza kulia) akiwa na wafukuza upepo wenzake kabla ya kuanza kutimua vumbi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni