·Waziri Mkuu Sera tabaani
· Mahakama Kamba Wanaume, Wanawake nusu fainali
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu za Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume na Kamba Wanawake zimetoa vipigo vikali leo tarehe 8 Octoba, 2023 kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa.
Mahakama Sports Kamba Wanaume waliwaburuta Mambo ya Ndani na kuwatupa kolokoloni, huku Wanawake ikiwabutua Waziri Mkuu Sera na kuwafungashia vilago kwenye mashaindano hayo.
Michezo yote miwili
imechezwa majira ya jioni saa 11:00 katika viwanja vya Mkwawa na kushuhudiwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Mkurugenzi wa Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Erasmus Uisso.
Ulikuwa mchezo wa Kamba Wanawake
ulioanza kuchezwa huku Waziri Mkuu Sera wakiingia uwanjani kwa kujiamini. Mchezo
huo ulikuwa kama wa kisasi kwa kuzingatia kuwa katika mashindano ya SHIMIWI
mwaka jana timu hizo ziliingia kwenye hatua kama hiyo na Waziri Mkuu Sera
ikanyonyolewa.
Baada wa waamuzi kuamuru
mchezo kuanza, Mahakama Sports kama kawaida yao hawakuwa na subira na walitembeza
kichapo kikali cha kufa mtu na kuwafanya timu pinzani wapoteane.
Hadi mivuto yote
ilipokamilika, Mahakama Sports ikazoa pointi zote mbili na kuwaacha wapinzani
wako hoi tabaani wakipumua juu juu kama paka aliyenasa kwenye matope, hivyo
kutupwa nje ya mashindano.
Baada ya mchezo huo
kukamilika, ulifuata mchezo wa Kamba Wanaume ambapo Mahakama Sports ilipangwa kupigishana
kwata na timu ya Mambo ya Ndani. Mchezo huo pia ulikuwa ni wa kisasi kwa kuzingatia
kuwa katika michezo ya Mei Mosi iliyopita, Mambo ya Ndani iliwapigisha chafya Mahakama.
Katika mchezo wa leo,
Mahakama Sports walionekana tangu mwanzo kukamia na waamuzi walipoamuru ‘ngoma”
iwekwe uwanjani, Mambo ya Ndani walikiona cha moto, kwani walipigwa kama ngoma
na kusweka kolokoloni katika mvuto wa kwanza.
Ilipofika katika hatua ya
pili, Mambo ya Ndani walijaribu kutumia mbinu ya kukaa chini ili kuwakata pumzi
vijana wa professa. Hata hivyo, kilichowatokea hawakuamini macho yao.
Mambo ya Ndani waliburutwa
vibaya na kujikuta wengine wanageukia kule walikotoka. Hadi mpambano unamalizika,
Mahakama Sports ikazoa pointi zote mbili na kutinga katika hatua ya nusu
fainali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni