Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor hivi karibuni alikutana
na kuzungumza na Mahakimu wote wa Mahakama katika Kanda yake kukumbushana
uwajibikaji na kupeana mikakati ya utoaji huduma ya haki kwa wananchi.
Kikao hiko kilichofanyika
kwenye Ukumbi wa Mkutano katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) kilihudhuriwa
na Majaji, Naibu Msajili na Mtendaji ambao kwa nyakati tofauti walipata wasaa
wa kuongea na Mahakimu hao.
Akizungumza katika kikao
hicho, Mhe. Mansoor alisema kuwa angependa Hakimu atambulike zaidi kupitia
uwajibikaji mzuri na sio vinginevyo.
“Wote hapa tumekasimiwa
mamlaka ya kutoa haki kwa wananchi na sio vinginevyo, ni rai yangu tufanye
jukumu hilo kwa uadidilifu usio tia mashaka, weredi mkubwa na wote tuwajibike
kwa usahihi” alisema Jaji Mfawidhi.
Naye Jaji Messe Chaba alizugumzia
suala la mashauri ya mirathi na kuwataka Mahakimu kuweka mikakati bora ya namna
ya kuwaelekeza wasimamizi wa mirathi mara shauri linapomalizika.
Aliongeza kuwa takwimu
zinaonesha uwepo wa kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti ya Mahakama Kanda ya
Morogoro na zinasubiri kulipwa kwa wanufaika wa mirathi.
“Tuwasaidie wahusika kubainisha
taarifa zao sahihi ili mafao yaweze kuwafikia wanufaika kwa wakati,” alieleza na
kusisitiza wale waliopewa jukumu la kukagua nyaraka za mashauri ya mirathi
kufanya kazi hiyo ipasavyo.
Kwa upande wake, Jaji Gabriel
Malata aliwahimiza Mahakimu kuiishi salamu ya Mahakama ya Tanzania inayosema “Uadilifu,
Weredi na Uwajibikaji” na kila mmoja kutambua mamlaka aliyopewa.
Aliwaeleza Mahakimu hao
kutogeuza mafaili yaliyopo mezani kwao kuwa fulsa ya kupenyeza mianya ya rushwa.
Naibu Msajili, Mhe.
Agustina Mmbando alipalilia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
na kusema hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Mahakama, hivyo
aliwataka maafisa hao kuishi kimkakati.
“JSDS sasa hivi
imeboreshwa na sasa tunaenda kwenye mfumo mpya wa usajili wa mashauri wa CMS
ambao tayari umefanyiwa majaribio na hii ni kwa Mahakimu wote nchi nzima,” alisema.
Katika kikao hicho, wajumbe walitumia nafasi hiyo kuwachagua Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Kanda ya Morogoro na Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Kihonda, Mhe. Kisaka Ramadhani alichaguliwa kuwa Mwenyekiti.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akizungumza wakati wa
kikao. Kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda hiyo, Mhe. Messe Chaba.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akizungumza wakati wa kikao.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata akizungumza wakati wa kikao.
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando akifuatilia hoja wakati
wa kikao.
Sehemu ya washiriki wa
kikao.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji
Mdawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati)
pamoja na Majaji Messe Chaba (kushoto) na Gabriel Malata (kulia) wakiwa katika
picha ya pamoja na washiriki wa kikao hicho.
Mwenyekiti wa JMAT Kanda ya Morogoro, Mhe. Kisaka Ramadhani akisoma taarifa fupi mara baada ya kuchaguliwa.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji
Mdawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati)
pamoja na Majaji Messe Chaba (kushoto) na Gabriel Malata (kulia) wakiwa katika
picha ya pamoja na Viongozi wa JMAT Kanda ya Morogoro mara baada ya kuchaguliwa.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji
Mdawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati)
pamoja na Majaji Messe Chaba (kushoto) na Gabriel Malata (kulia) wakiwa katika
picha ya pamoja na wawakilishi wa Kanda ya Morogoro katika mkutano mkuu wa JMAT
unaotegemea kufanyika mwezi Desemba huko jijini Dodoma.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni