Jumatatu, 9 Oktoba 2023

USIMAMIZI IMARA WA MAADILI YA WATUMISHI WA MAHAKAMA UNATEGEMEA KAMATI ZA MAADILI: JAJI MKUU

 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema usimamizi imara wa maadili ya Maafisa Mahakama unategemea taarifa za Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na wilaya.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na Wilaya katika Mkoa wa Kagera, Jaji Mkuu amesema Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kutokana na uchache wao ukilinganisha na ukubwa wa nchi, hawawezi kusimamia nidhamu na maadili ya Maafisa Mahakama peke yao hivyo Tume imekasimu majukumu yake kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.

Alisema uhai wa maadili ya Watumishi wa Mahakama unategemea sana taarifa zinazowasilishwa na Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya  ambazo Tume huzitumia ili kufahamu uhalisia wa hali ya maadili kwenye Mahakama zote nchini.

Alitoa wito kwa wajumbe wa Kamati za maadili ya Maafisa Mahakama kusimamia kikamilifu nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama ambao jukumu lao la msingi ni kutoa haki.

”Haki isiyoendana na maadili mema siyo haki, asilimia 99 ya haki inajengwa kwenye maadili hivyo bila ya kuwa na maadili huwezi kusema unatoa hki”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema lengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama kufanya ziara mkoani Kagera ni kubadilishana uzoefu wa kazi ya usimamizi wa nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama na wajumbe wa Kamati za Maadili, kusikiliza changamoto mbalimbali.

Aidha, Jaji Mkuu ameiomba Serikali mkoani Kagera kutoisahau Mahakama ya Tanzania inaposogeza huduma zake kwa wananchi zikiwemo miundombinu ya Tehama, umeme na nyumba za watumishi.

Awali akitoa mada katika Mkutano wa Tume na Watumishi wa Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta aliwataka watumishi hao kutambua na kuyaepuka  matendo yanayoweza kuwaingiza kwenye migogoro inayosababishwa na ukosefu wa nidhamu na maadili.    

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.

Aidha, Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 kimeiruhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni; Kamati ya Maadili ya Majaji, Kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya Mkoa na Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ya wilaya.

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mkoa na wilaya (hawapo pichani) katika mkoa wa Kagera leo tarehe 9 Oktoba, 2023. 
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mkoa na wilaya wakiwa katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama unaolenga kuziimarisha Kamati hizo.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mkoa na wilaya wakiwa katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama unaolenga kuziimarisha Kamati hizo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta akitoa mada kwenye Mkutano wa Tume na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mkoa na wilaya katika Mkoa wa Kagera leo tarehe 9 Oktoba, 2023. 
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa Tume na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba leo tarehe 9 Oktoba, 2023. 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni