Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama Bukoba
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wa Mahakama
kanda ya Bukoba kwa kutoa huduma bora na kuongeza kasi katika ya matumizi ya
Tehama iliyowezesha kusajili mashauri kwa njia ya mtandao kwa zaidi ya asilimia
99.
Akizungumza na watumishi wa kanda hiyo wakati wa Mkutano
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na watumishi hao jana mjini Bukoba, Jaji Mkuu
amesema mafanikio hayo yanadhihirisha ni kwa jinsi gani Mahakama inahama kwenda
kidigitali katika shughuli zake za utoaji haki.
Alisema Mahakama ya Tanzania imefanya mabadiliko makubwa
katika mfumo wa Usimamizi na Uendeshaji wa Mashauri (E-Case Management) na hivi
sasa mfumo huo uko katika hatua za mwisho za majaribio kabla ya kuanza kutumika
rasmi Tarehe 1 Novemba mwaka huu.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka watumishi wa Mahakama kote
nchini kuupitia mfumo huo mpya na kutoa mapendekezo ya maeneo yenye changamoto
yanayotakiwa kufanyiwa uboreshaji ili mfumo huo ufanye kazi vizuri kama ilivyokusudiwa.
”Mfumo huu utakapoanza kutumika utakuwa na faida nyingi
zikiwemo kuongeza ufanisi, kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko ya wananchi,
kupunguza hisia za kuwepo kwa vvitendo vya rushwa kutokana na uwazi na kusaidia
viongozi katika usimamizi”, alisema Jaji Mkuu.
Mwenyekiti huyo wa Tume pia amewataka watumishi wote wa
Mahakama nchini kuisoma kwa kina taarifa ya utafiti ya mwaka 2023 uliofanywa na
Taasisi ya Repoa kuhusu viwango vya wananchi kuridhika na huduma zinazotolewa
na Mahakama ili waweze kujitathmini zaidi kuhusu utendahji kazi wao na
kuyafanyia kazi baadhi ya maeneo yaliyoanishwa kwenye utafiti huo.
”Someni kwa kina taarifa ya utafiti uliofanywa na Repoa
ya mwaka 2023 na ile ya mwaka 2015 iliyotusaidia kuandaa Mpango Mkakati wa
miaka mitano wa Mahakama na pia someni taarifa ya utafiti ya mwaka 2019
iliyopima nusu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati huo, taarifa ya sasa inapima
nusu ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa awamu ya pili”, alisisitiza.
Aliwataka watumishi wa Mahakama kulipa uzito suala la
uadilifu kwa kuwa taarifa ya utafiti uliofanyika mwaka 2023 inaonesha kuwa
uadilifu umeimarika mahakamani lakini
bado kuna changamoro katika Mahakama za chini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni