Jumanne, 10 Oktoba 2023

MAHAKAMA DODOMA YAFANYA MAFUNZO KWA VITENDO KUHUSU MFUMO MPYA

Na Arapha Rusheke, Mahakama Kuu, Dodoma

Mahakama Mkoa wa Dodoma jana tarehe 9 Octoba, 2023 iliendesha mafunzo kwa vitendo kwa watumishi ili kuwajengea uelewa wa matumizi sahihi ya mfumo mpya ulioboresha (E-Advanced Case Management) wa kupokea na kuratibu mashauri yote yanayopokelewa mahakamani.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Adam Mambi katika ukumbi wa mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma. 

Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Mambi aliwataka washiriki kusikiliza kwa makini ili waweze kuuelewa mfumo huo mpya ambao umeboreshwa kufuatilia mwenendo wa shauri tangu linapofunguliwa hadi kumalizika kwake. 

“Huu ni mfumo mpya, tuna hama kutoka katika mfumo wa mwanzo wa JSDS II na sasa tunaenda kwenye mfumo wa kisasa wa E-case Management. Hii itarahisisha wananchi kupata kitu chochote cha Mahakama kwa urahisi kabisa,” alisema. 

Kaimu Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa kuanzishwa kwa mfumo huo mpya ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Jaji Mkuu na mpango mkakati wa Mahakama. 

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na watumishi katika Mkoa wa Dodoma, wakiwemo kutoka Mahakama Kuu Dodoma, Mahakama za Wilaya Bahi, Kongwa,Chemba, Mpwapwa na Kondoa. 

Kwa upande wa Mahakama Kuu, waliohudhuria ni Majaji, Naibu Msajili, Mtendaji, Afisa Utumishi na wengine huku kutoka katika kila Wilaya alikuwepo Hakimu Mfawidhi, Afisa Utumishi pamoja na Karani. 

Alikuwepo pia Afisa Tehama, Bi. Amina Said kutoka Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, ambaye ndiey alikuwa mtoa mada mkuu katika mafunzo hayo.

 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa vitendo kuhusu mfumo mpya ulioboreshwa wa kuratibu mashauri.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylvia Lushasi akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo.

Mtendaji wa Mahakamu Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Bw.Sumera Manoti (aliyesimama) akzungumza wakati wa mafunzo hayo.

 

Sehemu ya washiriki waliohudhuria mafunzo hayo wakifuatilia mafunzo hayo.

 

Mkufunzi, Bi. Amina Said akieleza jambo wakati wa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama Mkoa wa Dodoma.

 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.

 

Mtendaji wa Mahakamu Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti akifuatilia kwa umakaini  mafunzo ya E-Case management.

 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe Sylvia Lushasi (wa kwanza kushoto) akiwa na Mtunza Kumbukumbu Mwandamiz,i Bi. Fatmah Nkamirwa wakati wa mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni