Jumanne, 10 Oktoba 2023

WADAU WATAMBUA MCHANGO WA MAHAKAMA KATIKA JAMII



  Na Francisca Swai, Mahakama – Musoma.

Blogu ya DIMA online yatambua na kupongeza mchango wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, kwa jamii. 

Blogu hiyo ya DIMA Online inayotoa habari na elimu mbalimbali kwa jamii yenye ofisi zake Wilayani Tarime Mkoani Mara imetambua mchango huo kwa kutoa cheti cha pongezi kwa Mahakama hiyo.

Akikabidhi cheti hicho, kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya,  tarehe 9 Oktoba, 2023 Mwandishi wa Habari kutoka katika blogu hiyo Bi. Joviana Masano, alisema cheti hicho kimetolewa ikiwa ni ishara ya pongezi na kutambua mchango wa Mahakama katika utoaji wa elimu kwa umma.

“Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imekuwa ikitoa ushirikiano kwa wadau na jamii pale inapohitajika kufanya hivyo bila kusita,” Bi. Joviana alisema, huku akitolea mfano namna Mahakimu wanawake Mhe. Eugenia Rujwahuka na Mhe. Prisca Mkeha walivyoshirikiana na blogu hiyo katika kutoa elimu kwa jamii Wilayani Tarime wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwezi Machi ,2023 pamoja na namna Mhe. Bahati Bwire alivyoshiriki katika kutoa elimu katika mkutano wa wananchi wa mtaa wa Mtakuja A, kata ya Mwisenge iliyoko Musoma Mjini mwezi Aprili, 2023.

Mwakilishi huyo kutoka blogu ya DIMA alisema elimu ya sheria inahitajika kwa jamii kwani wananchi wengi hawawezi kufika katika maeneo ya Mahakama kuitafuta, bali elimu inapowafuata walipo inakuwa msaada mkubwa kwao na kwa kufanya hivyo taratibu jamii zetu zinapata uelewa na kubadili fikra, mienendo na mzoea jambo linalosaidia kupunguza uhalifu na kuwasaidia hasa wanawake na watoto ambao wamekuwa wakikandamizwa na sheria nyingi za kimila.

Akipokea cheti hicho cha pongezi,  Mhe. Jaji Mtulya, aliushukuru  uongozi  huo,  kwa kutambua mchango wa Mahakama katika jamii. Ambapo alisema ‘mrejesho kama huu kutoka kwa wadau unaisaidia Mahakama kutambua namna inavyowafikia wananchi na kuona wapi waboreshe zaidi ili wananchi waweze kupata uelewa sahihi wa masuala mbalimbali ya kisheria,’alisema.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya, aliwashukuru DIMA online kwa namna wanavyoshirikiana na Mahakama katika mambo mbalimbali kama hayo ya utoaji elimu na hasa katika maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini.

Cheti cha pongezi kilicho kabidhiwa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma kutoka Blogu ya DIMA online.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (wa kulia) akipokea cheti cha pongezi kutoka Mwandishi wa Habari kutoka blogu ya DIMA   online Bi. Joviana Masano (wa pili kushoto) wengine ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa kwanza kulia) pamoja na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Erick Marley.

 

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo – Mahakama).

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni